AFC Leopards warukia nafasi ya 10 baada ya kutoka sare
MABINGWA mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), AFC Leopards, waliokota Jumatano alama moja iliyowakweza hadi nafasi ya 10 jedwalini baada ya kuwalazimishia Kariobangi Sharks sare ya 1-1 uwanjani Kasarani.
Wyvonne Isuza aliwaweka Leopards kifua mbele kunako dakika ya kwanza kabla ya Sharks waliomaliza mchuano wakiwa na wachezaji 10 ugani kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili.
Kariobangi Sharks walipata pigo katika dakika 62 pale Ian Taifa alipolishwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya mlinzi wa Ingwe Isaac Kipyegon baada ya refa kumwonya mara kadhaa
Nguvu mpya George Abege ndiye aliwafungia Kariobangi Sharks katika dakika za lala salama.
Sajili mpya Paul Were alimmegea Isuza, ambaye anaongoza orodha ya wafungaji wa Ingwe msimu huu, kwa mabao sita pasi safi na kumwezesha kufunga bao hilo mwanzo wa mechi.
Chini ya mkufunzi Casa Mbungo, Leopards kwa sasa wanajivunia alama 31, mbili pekee nyuma ya Sharks ambao wanafunga mduara wa tisa-bora baada ya kutandaza jumla ya michuano 25.
Nafuu zaidi kwa Leopards ambao kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Bandari FC wikendi hii, ni kwamba Sharks ya kocha William Muluya imesakata mchuano mmoja zaidi kuliko wao.
Baada ya kumenyana na Bandari ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 45, Leopards wameratibiwa kuchuana na Nzoia Sugar, Mathare United na Zoo Kericho kwa usanjari huo.
Kwa upande wao, Sharks watashuka dimbani kuchuana na Posta Rangers wikendi hii, kabla ya kuvaana na Chemelil Sugar na Kakamega Homeboyz mtawalia.
KCB wazamishwa
Katika mchuano wa Jumatano, chombo cha wanabenki wa KCB kilizamishwa na Chemelil Sugar kwa kichapo cha mabao 2-1 uwanjani Kenyatta, Machakos.
Chemelil kwa sasa wanakamata nafasi ya 14 kwa alama 28, moja nyuma ya KCB ambao wana idadi sawa ya pointi na Nzoia walioagana na Western Stima kwa sare tasa ugani Sudi, Bungoma.
Mchuano kati ya Stima na Nzoia ulikuwa wa kwanza kwa kocha Godfrey ‘Solo’ Oduor kusisimia tangu aaminiwe kudhibiti mikoba ya Nzoia ambao wanalenga kumaliza kampeni za muhula huu ndani ya mduara wa tisa-bora.
Stima wanashikilia nafasi ya 11 kwa alama 30, moja pekee kuliko KCB.
Kwingineko, Ulinzi Stars walipaa hadi nafasi ya sita hapo Jumatano baada ya kuwakomoa Vihiga United 1-0 uwanjani Afraha, Nakuru.
Mabingwa hao mara nne wa KPL kwa sasa wanajivunia alama 36, tano pekee nyuma ya Kakamega Homeboyz wanaofunga mduara wa nne-bora.
Matokeo
Sharks 1-1 Leopards, KCB 1-2 Chemelil Sugar, Nzoia 0-0 Western Stima, Ulinzi Stars 1-0 Vihiga Utd.