Michezo

AFC Leopards yaandaa bonge la sherehe ya ‘Ingwe@60’

March 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN ASHIHUNDU

MAANDALIZI ya kuadhimisha miaka 60 tangu kuasisiwa kwa klabu ya AFC Leopards almaarufu ‘Ingwe’ yanazidi kunoga huku kamati andalizi ikiahidi kuwakata kiu mashabiki wa klabu hiyo kongwe.

Akizungmza na Taifa Spoti mnamo Jumatatu, mwenyekiti wa kamati andalizi ya ‘Ingwe@60’ Vincent Shimoli alisema kutakuwa na burudani ya kila aina kuanzia Machi 22 hadi Machi 24, 2024, ambayo ndio itakuwa siku ya kilele cha tamasha hizo zitakazofanyika katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo.

Alisema Ingwe imealika timu ya AE Ramassa kutoka Uhispania kwa mechi ya kirafiki kuadhimisha siku hiyo kuu.

Kabla ya mechi hiyo, waandalizi na mashabiki watajihusisha katika shughuli za kijamii kama vile kupanda miche ya miti, na kutembelea watoto walio katika makao ya watoto.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja akiwa na Mlezi wa klabu ya AFC Leopards Alex Muteshi, mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda na Mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya ‘Ingwe@60’Vincent Shimoli walipokutana jijini Nairobi mnamo Ijumaa. PICHA | JOHN ASHIHUNDU

Wakati wa sherehe hiyo muhimu, Bw Shimoli alisema mashabiki watakaomiminika uwanjani humo watatumbuizwa na wasanii maarufu kwa vibao motomoto.

Baadhi ya wasanii wanaotarajiwa kutumbuiza ni Eammanuel Musindi, Naftali Shitoka, Vincent Ongidi, Freddy Tolo Akivambo, na David Barasa wa Webuye Jua Kali.

Alisema huenda Diamond Platnumz kutoka taifa jirani la Tanzania akaalikwa pia.

Kwa ujumla, mashabiki wa watapata burudani moja baada ya nyingine sambamba katika hitimisho hilo la Sikukuu ya Kuzaliwa kwa Ingwe.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja ni miongoni mwa watu mashuhuri waliotoa michango ya pesa taslimu kufanikisha sherehe hiyo.

Kutoka Kushoto: Mlezi wa klabu ya AFC Leopards Alex Muteshi, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda na Mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya ‘Ingwe@60’Vincent Shimoli walipokutana jijini Nairobi mnamo Ijumaa. PICHA | JOHN ASHIHUNDU

Bw Sakaja ambaye aliwahi kuwa mlezi wa klabu hiyo inayojivunia wafuasi wengi nchini, alitoa Sh2 milioni kugharimia maandalizi.

Ingwe inajivunia mataji 12 ya Ligi Kuu ya Kenya, ubingwa mara 10 wa Kombe la FKF, na mataji matano ya CECAFA miongoni mwa mengine.

Akitoa shukran kwa msaada wa Bw Sakaja, Bw Shimoli alitoa wito kwa viongozi wengi kujitokeza kupamba siku hiyo muhimu kwa klabu.