Michezo

AFCON: Fataki Nigeria, Cameroon wakionana katika 16-bora

July 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

ALEXANDRIA, Misri

TIMU mbili maarufu zaidi barani Afrika, Nigeria na Cameroon zitaonana ana kwa ana Jumamosi usiku kwenye mtanange wa 16-bora wa Kombe la Afrika (AFCON) unaotarajiwa kuibua mihemko mikali.

Vikosi hivyo kutoka Afrika Magharibi vilimaliza katika nafasi za pili kwenye makundi yao. Nigeria walikuwa katika Kundi B wakati Cameroon wakipangwa katika Kundi F.

Kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, hali imekuwa ngumu kwa Nigeria ikiwa pamoja na kukosa kufuzu kwa michuano hii mikubwa zaidi barani Afrika.

Fainali za mwaka 2019 ndizo za kwanza kushiriki tangu wanyakue ubingwa wa taji hilo mnamo 2013, baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali za awali.

Licha ya hayo ni muhimu kukumbuka kwamba kila wanaposhiriki, wanakuwa moto wa kuotea mbali, ikizingatiwa kuwa wametinga nusu-fainali mara 11 katika mechi 12 iliyopita, na ni mwaka wa 1982 pekee ambao walikosa kufika angalau robo-fainali.

Mwaka huu, kichapo cha 2-0 kutoka kwa Madagascar inayoshikilia nafasi ya 63 duniani kinawapa mashabiki wao wasiwasi, ingawa walishinda Burundi na Guinea katika mechi nyingine mbili.

Nigeria walimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Madagascar lakini itakumbukwa kuwa kufikia sasa, vijana hao wa kocha Gernot Rohr wameshindwa mara mbili pekee katika mechi 12 tangu wabanduliwe nje ya fainali za Kombe la Dunia.

Tatizo kuu la kikosi hiki katika mechi za karibuni ni kushindwa kufunga mabao, lakini kocha wao amesema amerekebisha makosa hayo.

Kama ilivyo kwa Nigeria, Cameroon wanafikiria walifaa kuongoza kundi lao ambalo vinara walikuwa majirani zao Ghana.

Kikosi imara

Kocha Rohr ameahidi kuteremsha uwanjani kikosi imara akikumbuka kwamba mechi kati ya mataifa haya mawili ni kama fainali.

“Dhidi ya Madagascar ilibadilisha kikosi kwa sababu nilitaka wachezaji kadhaa wa akiba wapate nafasi kuonyesha vipaji vyao hadharani,” alisema Mfaransa huyo.

“Mechi itakuwa ngumu, kwa sababu kuna tofauti ndogo baina ya timu hizi mbili, hivyo lazima tujipange vyema kwa kibarua hiki,” aliongeza.

Zilipokutana mwaka uliopita ugani Godswill Akpabio katika mechi ya mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia, Nigeria waliibuka na ushindi wa 2-0.

“Tumekuwa na siku nyingi kupumzika, na kila mchezaji kambini wanaisubiri kwa hamu mechi ya leo,” alisema.

Cameroon waliokuwa kwenye Kundi C walitarajiwa kumaliza wa kwanza, lakini wakapata pointi nne pekee kutokana na sare ya 0-0 na Benin ambao pia walifuzu kwa hatua ya 16 bora.

Katika mechi hiyo, Cameroon walitawala na kumiliki mchezo kwa asilimia 72 na makombora 11 ambayo yalikaribia kuingia. Ushindi wao wa 2-0 katika mechi ya utangulizi dhidi ya Guinea-Bissau uliwasaidia katika juhudi zao za kufuzu baada ya kutofungwa bao.