Afcon: Mataifa yaliyodunishwa yahangaisha mibabe
NA JOHN ASHIHUNDU
TIMU zinazochukuliwa kuwa ni ndogo ambazo wengi walitarajia kuziona zikipigwa kwa mabao mengi katika mashindano ya kusaka Taifa Bingwa Afrika (Afcon 2023) yanayoendelea nchini Cote d’Ivoire, zimeshangaza wengi baada ya kukabiliana vilivyo na vigogo.
Baada ya wenyeji Cote d’Ivoire kushinda Guinea Bissau 2-0 katika mechi ya ufunguzi, mechi zilizofuata zilikuwa na upinzani mkali na kushangaza wengi ambapo hadi mwishoni mwa mechi hizo za kwanza, ni watetezi tu Senegal waliopata ushindi wa 3-0 dhidi ya limbukeni Gambia.
Nigeria walikumbana na kibarua kigumu dhidi ya Equatorial Guinea katika mechi iliyomalizika kwa 1-1.
Cape Verde iliyofikiriwa kuwa rahisi mbele ya Ghana iliduwaza wengi baada ya kushinda mechi hiyo kwa 2-1, huku Msumbiji ikiibana Misri ya Mohamed Salah kwa 2-2.
Mbali na vigogo hao, matokeo mengine ya kushangaza yalikuwa Misri 2 Msumbiji 2, Cape Verde 2 Ghana 1, Cameroon 1 Guinea 1, Algeria 0 Namibia 1.
Licha ya kucheza vizuri, Tanzania walichapwa 3-0 na Morocco, lakini kuna matumaini ya vijana hao wa Taifa Stars kufanya vizuri katika mechi mbili za ‘Kundi F’ watakapocheza na DR Congo na baadaye Zambia.
Kocha Adel Amrouche anapaswa kukaa na kamati yake ya kiufundi kupanga mikakati mufti kwa lengo la kuhakikisha Taifa Stars imepata matokeo mazuri katika mechi hizo, hata kama haitafuzu kutoka Kundi hilo la F.
Lazima ikumbukwe kwamba Morocco iliyo na mastaa kadhaa walio na ujuzi wa miaka mingi walipata ushindi kwa sababu walikuwa wamejiandaa vyema kiakili, ingawa pia baadhi ya mashabiki walilalamika kulikuwa na uonevu wa waamuzi.
Mashabiki wa Tanzania lazima waendelee kuisapoti timu hiyo katika mechi zilizobakia, badala ya kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuishambulia, ikizingatiwa kwamba timu haiwezi kujengwa kwa siku moja.
Lazima ikumbukwe kwamba Morocoo ni timu iliyofika katika nusu-fainali ya Kombe la Dunia, mbali na kuwa katika nafasi ya 11 kwenye viwango vya ubora Duniani, wakati Tanzania ikiorodheshwa katika nafasi ya 127.
Kikosi cha Tanzania kina vijana wa umri mdogo ambao wana muda wa kujijenga ili kiwe na ushindani mkubwa, hasa wakati huu taifa hilo linajiandaa kuungana na Kenya pamoja na Uganda kuandaa fainali za Afcon 2027.