• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
AFCON: Mataifa yaliyojipanga kwa mtanange Vs yale yanayochangisha fedha

AFCON: Mataifa yaliyojipanga kwa mtanange Vs yale yanayochangisha fedha

Na GEOFFREY ANENE

MATAIFA mengi yanayoshiriki Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri mwaka 2019 yametangaza motisha ya kifedha kwa timu zao za kitaifa yakitumai watajituma vilivyo kuandikisha historia.

Harambee Stars iko katika orodha ya timu zilizopigwa jeki na serikali ya Kenya ilipotengewa Sh244 milioni kwenye bajeti. Mataifa mengine kama Zimbabwe, Guinea na Burundi yalilazimika kuomba wananchi kuchangisha fedha kupitia harambee nayo Nigeria iliwacha watu vinywa wazi waziri wake mmoja alipofichua kwamba ilisahaulika katika bajeti ya mwaka huu. Safari yetu inaanza na Kundi C, ambalo liko na Kenya, Algeria, Senegal na Tanzania.

KUNDI C:

Algeria: Nchi ya Algeria ni mojawapo ya mataifa yaliyotengea wachezaji wake fedha za kudondosha mate. Hata hivyo, mabingwa hawa wa mwaka 1990 watalazimika kujituma zaidi kupata marupurupu hayo. Ripoti zinasema kwamba kila mchezaji atatuzwa Sh11.4 milioni Algeria ikifika nusu-fainali, Sh48.1 milioni ikizoa nishani ya fedha na Sh68.7 milioni ikitwaa taji. Timu hii inayofahamika kwa jina la utani kama ‘The Fennecs’, ‘Desert Foxes’ ama ‘Desert Warriors’, inashikilia nafasi ya 68 duniani katika viwango vya ubora vilivyotangazwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mnamo Juni 14.

Kenya: Kila mchezaji aliyetajwa na kocha Sebastien Migne katika kikosi cha wachezaji 23 atatia mfukoni angaa Sh750, 000, Rais wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Nick Mwendwa alisema majuma machache yaliyopita. Wachezaji pia watazawadiwa Sh250,000 kila mmoja kwa kushinda mechi. Serikali iliidhinisha bajeti ya Sh244 milioni mwezi Machi, ingawa kabla ya Harambee Stars kutoka katika kambi ya mazoezi nchini Ufaransa hapo Juni 18, Mwendwa alisema timu imepokea marupurupu pekee. “Bado hatujapata bonasi. Tunazungumza na serikali.” Vijana wa Migne wanashikilia nafasi ya 105 duniani baada ya kuruka Libya na Madagascar.

Senegal: Ripoti kutoka jijini Dakar zinasema kwamba Teranga Lions iligawana Sh40.5 millioni baada tu ya kujikatia tiketi ya AFCON. “Wachezaji 41 waliotumiwa katika mechi za kufuzu za AFCON watagawana Sh1.2 milioni kila mmoja ya kufuzu. Senegal ni ya kwanza barani Afrika katika nafasi 22 duniani.

Tanzania: Mwezi Machi baada ya Tanzania kurejea katika AFCON tangu mwaka 1980, Rais wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli alitunukia kila mchezaji wa Taifa Stars kipande cha ardhi mjini Dodoma. Taifa Stars inashikilia nafasi ya 131 duniani.

KUNDI A:

Misri: Washikilizi hawa wa rekodi ya mataji mengi ya AFCON wana kiwango kilichopitishwa na Shirikisho la Soka nchini Misri (EFA). Shirikisho hili litapatia kila mchezaji Sh86, 750 katika kila mechi, Sh127,387 kwa kufika robo-fainali, Sh193,629 (nusu-fainali) na Sh285,348 (fainali) jinsi ilivyokuwa katika makala ya mwaka 2017.

DR Congo: Timu ya DR Congo almaarufu Leopards iligonga vichwa vya habari kwa sababu mbaya katika makala ya mwaka 2017 Waziri wa Michezo Willy Bakonga alipolazimika kuabiri ndege hadi nchini Gabon kusuluhisha mgomo kuhusu marupurupu kupunguzwa siku tatu kabla ya mashindano kuanza.

Uganda: Rais wa Uganda Yoweri Museveni alituza Cranes (wachezaji na benchi la kiufundi) Sh102 million (Sh3.7 bilioni za Uganda) kwa kuingia AFCON 2019. Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA) halikufichua kila mtu atapokea kiasi gani cha fedha hizo, ingawa kila mchezaji alifurahishwa na Sh600,000 kwa kupiga Lesotho nyumbani na ugenini katika mechi za kufuzu.

Zimbabwe: Rais Emmerson Mnangagwa alilazimika kuuza skafu yake katika harambee zaidi ya wiki moja iliyopita jijini Harare. Ilinunuliwa kwa Sh3.3 milioni katika harambee hiyo iliyolenga kuchangisha Sh51 milioni. Wachezaji wa Zimbabwe walizawadiwa Sh153,000 (marupurupu), Sh510,000 (kuwa kikosini) na Sh612,000 (kushinda mechi) mwaka 2017. Walitaka bonasi ya kushinda mechi iongozwe kwa Sh204, 000.

KUNDI B:

Nigeria: Waziri wa zamani wa michezo wa Nigeria, Solomon Dalung alishangaza wengi wiki moja iliyopita alipolaumu Shirikisho la Soka nchini humo (NFF) kwa “kukosa kujumuisha bajeti ya AFCON 2019 katika bajeti waliyowasilisha kwa serikali.” Super Eagles hutunuku wachezaji Sh510, 000 kwa kila ushindi katika raundi ya kwanza.

Guinea: Mwezi Aprili mwaka 2018, Shirikisho la Soka nchini Guinea (FEGUIFOOT) ilisaini kandarasi ya Sh51.3 milioni na kampuni ya Macron. Kampuni hii ya mavazi ya michezo iliahidi kujadiliana na shirikisho hilo kuhusu bonasi ya wachezaji ikiwa Syli Nationale itaingia AFCON 2019. Ripoti zinasema kwamba Guinea iliunda kamati ya kuchangisha fedha hivi majuzi. Inasemekana kwamba harambee hiyo ilichangisha Sh5.3 milioni. Ingali inaitisha mchango zaidi.

Madagascar: Timu ya taifa ya Madagascar inayofahamika kwa jina la utani kama Barea ilizawadiwa Sh2.9 milioni na serikali ya nchi hiyo kwa kuingia AFCON kwa mara yake ya kwanza kabisa hapo Machi mwaka huu.

Burundi: Mwezi Mei, Rais wa Shirikisho la Soka nchini Burundi, Reverien Ndikuriyo aliitisha harambee kuchangia Swallows Sh10.2 milioni. Alisema kwamba Burundi haikuwa na fedha za kutosha kusaidia timu hiyo kuishi nchini Misri kwa mashindano ya AFCON yatakayodumu siku 29 nchini Misri. Wahisani wengi walijitokeza, huku ripoti zikisema kwamba Juni 13 pekee ilishuhudia Sh3 milioni zikichangishwa.

KUNDI D:

Morocco: Licha ya kubanduliwa nje ya Kombe la Dunia katika mechi za makundi mwaka 2018 nchini Urusi, mabingwa wa Afrika mwaka 1976 Atlas Lions walizawadiwa na Shirikisho la Soka nchini Morocco (FRMF) Sh2.1 milioni kila mchezaji.

Ivory Coast: Matunda ya bidii za mchwa za Elephants katika Kombe la Afrika mwaka 2015 ziliwezesha kila mchezaji kupokea nyumba ya bei ya Sh5.1 milioni kila mmoja pamoja na Sh4.7 milioni fedha taslim.

Afrika Kusini: Wachezaji wa Bafana Bafana walitia mfukoni Sh419,122 kila mmoja kwa kuchapa Libya 2-1 katika mechi ya mwisho ya Afrika Kusini ya kufuzu kushiriki AFCON mwaka 2019. Kiasi hiki ndicho bonasi ya kawaida ya Bafana Bafana.

Namibia: Wizara ya Michezo ya Namibia ilitangaza kufadhili Shirikisho la Soka nchini humo kwa Sh132.2 milioni kufanikishja ushiriki wa Brave Warriors katika AFCON nchini Misri. Kiasi hiki, ripoti zinasema, ni bonasi ya kufuzu, ushindi, kushiriki mechi pamoja na mahitaji mengine kwenye mashindano hayo.

KUNDI E:

Tunisia: Hakuna rekodi kuonyesha jinsi Tunisia inavyopatia kikosi chake cha Carthage Eagles motisha ya kifedha isipokuwa kujiuzulu kwa kocha George Leekens baada ya Kombe la Afrika mwaka 2015 akisema kwamba bado hawajalipwa bonasi zao. “Miezi minne baada ya mashindano, bado hatujalipwa bonasi yetu,” alisema Mbelgiji huyu wakati wa kujiuzulu kwake. Tunisia ni mabingwa wa mwaka 2004.

Mali: Mwaka 2010, Shirikisho la Soka nchini Mali (FMF) lilifutilia mbali marupurupu baada ya kusikitishwa na matokeo ya timu hiyo almaarufu kama Eagles. Miaka sita iliyopita, nyota wa Mali, Seydou Keita, ambaye alitamani sana kushinda taji na timu ya taifa, aliahidi kulipa wachezaji bonasi kwa kutumia fedha zake ikiwa shirikisho litashindwa kufanya hivyo.

Mauritania: Habari kuhusu mpango wa bonasi kwa timu ya taifa ya Mauritania haujakuwa wazi, ingawa Shirikisho la Soka nchini humo (FFRIM) mwezi Mei lilisaini kandarasi na kampuni ya vifaa vya michezo ya AB Sport. Mnamo Juni 15, Ahmed Yahya, rais wa FFRIM, alichapisha ujumbe kwenye mtandao wake wa Twitter akisema kwamba timu hiyo ilikuwa ikifadhiliwa na shirikisho hilo na kupata usaidizi kutoka kwa serikali na pia wananchi.

Angola: Kwa mujibu wa tovuti ya Correio da Mahna, Palancas Negras, timu ya taifa ya Angola inavyofahamika kwa jina la utani, itazawadiwa Sh1 milioni kila mchezaji ikifika raundi ya 16-bora, Sh1.5 milioni (robo-fainali) na Sh4 milioni kwa kubeba taji. Nafasi nzuri ambayo Angola imewahi kumaliza AFCON ni robo-fainali mwaka 2008 na 2010.

KUNDI F:

Cameroon: Indomitable Lions inafahamika sana kwa migomo ya wachezaji katika dakika ya mwisho. Mwaka 2014, Shirikisho la Soka la Cameroon (FECAFOOT) lililazimika kuchukua mkopo kwenye benki kulipa wachezaji kabla ya timu kuelekea nchini Brazil kwa Kombe la Dunia. Shirikisho hili lilikuwa na mpango maalum wa kuwapa wachezaji bonasi mwaka 2017. Kila mchezaji alitia mfukoni Sh7 milioni kwa kushinda AFCON miaka miwili iliyopita katika nchi jirani ya Gabon.

Ghana: Vyombo vya habari nchini Ghana viliripoti majuzi kwamba Rais Nana Akufo Addo ameahidi kurejesha mpango wa kutunuku kila mchezaji Sh1 milioni kwa kila mechi Black Stars inasakata kwenye AFCON 2019. Kiasi hicho kilikuwa kimepunguzwa hadi Sh0.5 milioni wakati wa makala yaliyopita nchini Gabon. Ripoti zinasema kwamba serikali ya Ghana imetengea mabingwa hawa mara nne wa Afrika Sh816 milioni.

Benin: Hakuna ripoti za kuonyesha jinsi Shirikisho la Soka nchini Benin (FEBEFOOT) linavyopongeza wanasoka wake wanaowakilisha taifa katika AFCON nchini Misri.

Guinea-Bissau: Mapema mwezi huu wa Juni, serikali ya Guinea-Bissau ilitangaza bajeti ya Sh87.7 milioni kwa timu yake ya taifa Djurtus.

You can share this post!

AFCON: Jiandaeni kwa kipute cha joto kali Misri – CAF

Maseneta wapinga sera ya serikali ya kuajiri wafanyakazi...

adminleo