Afcon: Senegal wakomoa Cameroon na kutinga hatua ya 16-bora
Na MASHIRIKA
MABINGWA watetezi wa Kombe la Afrika (Afcon), Senegal, walijikatia tiketi ya hatua ya 16-bora baada ya kupepeta Cameroon 3-1 katika ‘Kundi C’ uwanjani Charles Konan Banny jijini Yamoussoukro mnamo Ijumaa.
Ismaila Sarr aliwaweka Senegal kifua mbele kunako dakika ya 16 kabla ya Habib Diallo kufanya mambo kuwa 2-0 katikati ya kipindi cha pili.
Ingawa Jean-Charles Castelletto alirejesha Cameroon mchezoni katika dakika ya 83, Sadio Mane alifungia Senegal bao la tatu mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya George-Kevin Nkoudou kupoteza nafasi ya kusawazisha.
Senegal watamaliza kileleni mwa Kundi C iwapo wataepuka kichapo kutoka kwa Guinea katika mchuano wao wa mwisho kundini mnamo Jumanne.
Guinea kwa sasa wanakamata nafasi ya pili kundini kwa alama nne baada ya kucharaza Gambia 1-0, Ijumaa. Matokeo hayo yanamaanisha kuwa Cameroon sasa lazima wapige Gambia mnamo Jumanne ili wasonge mbele kutoka Kundi C.
Mabingwa hao mara tano wa Afcon wanajivunia alama moja pekee kutokana na mechi mbili na huenda bado wakafuzu kwa muondoano wakiwa miongoni mwa timu tatu bora makundini iwapo watashindwa kuangusha Guinea kwa wingi wa mabao.
Kipa Andre Onana aliwajibishwa na Cameroon michumani baada ya kukosa pambano lililokamilika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Guinea mnamo Jumatatu alipohiari kuchezea waajiri wake Manchester United dhidi ya Tottenham Hotspur katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) saa 24 kabla ya taifa lake kushuka dimbani.
Hata hivyo, mlindalango huyo mwenye umri wa miaka 27 alijipata lawamani kwa utepetevu uliochangia bao la kwanza la Senegal aliposhindwa kudhibiti mpira uliopigwa kwa kichwa na Pape Matar Sarr.
Kocha Aliou Cisse aliongoza Senegal kunyanyua taji lao la kwanza la Afcon miaka miwili iliyopita na miamba hao wanapania sasa kuwa kikosi cha kwanza kuhifadhi taji hilo tangu 2010 Misri ambao ni wafalme mara saba walipolitwaa kwa mara ya tatu mfululizo.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO