Afcon: Wenyeji Cote d’Ivoire kuvaana na Guinea-Bissau
NA MASHIRIKA
FAINALI za Kombe la Mataifa (Afcon) zitaanza kesho Jumamosi nchini Cote d’Ivoire, huku mataifa 24 yakikabiliana katika makundi sita.
Michuano hiyo ilipangwa kufanyika mwaka 2023, lakini ikaahirishwa hadi mwaka huu wa 2024 kutokana na msimu wa mvua kubwa iliyonyesha eneo la Afrika Magharibi linakopatikana taifa andalizi la Cote d’Ivoire.
Mashindano hayo yatakayomalizika Februari 11 yataanza kwa pambano la ufunguzi kati ya wenyeji Cote d’Ivoire na Guinea-Bissau ugani Alassane Quattara mjini Abidjan.
Harambee Stars ya Kenya haikushiriki katika mechi za mchujo wa kufuzu baada ya kufungiwa na Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) hapo awali Serikali ilipoingilia usimamizi wa soka mwishoni mwa 2021, lakini Afrika Mashariki itawakilishwa na Tanzania.
Kikosi cha Taifa Stars chini ya kocha wa zamani wa Harambee Stars Adel Amrouch kitaanza dhidi ya Morocco mnamo Jumatano juma lijalo, kabla ya kuvaana na Zambia (Januari 21) na kisha mabingwa mara mbili DR Congo mnamo Januari 24.
Timu hiyo iliyoandikisha ushindi wa 2-0 dhidi ya Misri katika mechi ya kupimana nguvu iliondoka Dar es Salaam Jumatatu kuelekea Cote d’Ivoire tayari kwa michuano hiyo. Hii itakuwa mara yao ya tatu baada ya awali kucheza fainali za 1980 nchini Nigeria na mnamo 2019 kule Misri.
Wenyeji Cote d’Ivoire, Nigeria, Senegal na Morocco ni miongoni mwa timu zinazojivunia mastaa lakini huenda zikakabiliwa na upinzani mgumu kutoka kwa timu zinazotafuta sifa.
Nigeria imekabiliwa na foka za mashabiki baada ya kutoka sare na na Lesotho pamoja na Zimbabwe katika mechi za mchhujo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia la 2026, lakini Victor Osimhen anaamini kikosi kipo imara kuvuma nchini Cote d’Ivoire.
“Tunajua nini tunahitaji ili kushinda Afcon. Tumejifunza zaidi kutokana na sare tulizopata dhidi ya Lesotho na baadaye Zimbabwe,” alisema kiungo Frank Onyeka wa kikosi hicho cha Super Eagles.
KUNDI A: Cote d’Ivoire, Equatorial Guinea, Guinea-Bissau na Nigeria.
KUNDI B: Cape Verde, Misri, Ghana na Msumbiji.
KUNDI C: Cameroon, Gambia, Guinea na Senegal.
KUNDI D: Algeria, Angola, Burkina Faso na Mauritania.
KUNDI E: Mali, Namibia, Afrika Kusini na Tunisia.
KUNDI F: DR Congo, Morocco, Tanzania na Zambia.
Ratiba, Jumamosi: Cote d’Ivoire na Guinea-Bissau (saa tatu usiku).
Jumapili: Nigeria na Equatorial Guinea (saa kumi na moja jioni), Misri na Msumbiji (saa mbili usiku), Ghana na Cape Verde (saa tatu usiku).
Uchambuzi wa ziada umefanywa na John Ashihundu