Aguero kusalia nje kwa miezi miwili zaidi kuuguza jeraha la goti
Na MASHIRIKA
KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City anahofia kwamba mshambuliaji matata Sergio Aguero atakosa mechi zote za miezi miwili ya kwanza kwenye kampeni za msimu huu wa 2020-21.
Aguero alipata jeraha baya la goti mnamo Juni 22, 2020 wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha na Burnley.
Jeraha hilo lilimweka fowadi huyo raia wa Argentina nje ya mechi zote 10 za mwisho wa muhula wa 2019-20 na pia michuano miwili ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti.
Guardiola kwa sasa amekiri kwamba hana uhakika iwapo Aguero ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Man-City atakuwa amerejea katika hali shwari ya kuchezeshwa kufikia Novemba.
“Tulijua kwamba jeraha hilo lilikuwa baya na lingemweka nje kwa kipindi kirefu. Atahitaji muda wa mwezi mmoja au miwili hivi kabla ya kuanza tena kutuchezea,” akasema kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich.
Kukosekana kwa Aguero katika kikosi cha kwanza cha Man-City kunatazamiwa kumpisha fowadi raia wa Brazil, Gabriel Jesus aliyefunga jumla ya mabao matano kutokana na mechi 12 za mwisho wa msimu uliopita.
Man-City kwa sasa wanajiandaa kwa gozi la EPL litakalowakutanisha na Wolves uwanjani Molineux mnamo Septemba 21, 2020. Guardiola atapania kumchezesha sajili mpya Ferran Torres katika mchuano huo ili ashirikiane na Raheem Sterling, Jesus na Bernardo Silva katika safu ya mbele.
Kubanduka kwa kiungo veterani David Silva ugani Etihad mwishoni mwa msimu jana kunamsaza Guardiola bila ya mchezaji yeyote aliyekuwa sehemu ya kikosi kilichovunia Man-City ubingwa wa EPL mnamo 2012. Silva, 35, aliyoyomea Real Sociedad ya Uhispania.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO