Ahadi nyingine yazama: Harambee Stars kucheza mechi za nyumbani Malawi
NA JESSE CHENGE
WAZIRI wa Michezo Ababu ametupia lawama serikali za awali kwa kushindwa kuboresha viwanja vya Kenya ambavyo vimepelekea nchi kulazimika kuandaa mechi zake za kimataifa katika nchi nyingine.
Namwamba ambaye awali aliahidi Wakenya kwamba Nyayo Stadium itakuwa tayari kuandaa michezo mwezi wa Juni ameelekeza lawama kwa serikali za awali.
Licha ya juhudi za kuboresha viwanja vya Nyayo na Kasarani na serikali ya Kenya Kwanza, Harambee Stars bado itacheza mechi zake za nyumbani nchini Malawi kufuatia viwanja hivyo kukosa kuafikia ubora wa kimataifa.
Namwamba ameeleza kusikitishwa kwake na hali ya miundombinu ya michezo nchini akidai kuwa kwa miaka 40 iliyopita imepuuzwa akisema kuwa viwanja vya Kisumu na Kericho ni viwanja vya kitaifa kwa jina tu na havikidhi viwango vya Fifa.
“Miundombinu ya michezo nchini kwa sasa haikidhi viwango,” Namwamba alisema wakati wa ziara yake katika Uwanja wa Masinde Muliro huko Kanduyi, Bungoma.
Akizungumzia hali isiyo ya kuridhisha katika Viwanja vya Jomo Kenyatta Kisumu na Kiprugut Kericho, miongoni mwa vingine, alisema kwamba vina viwango vya kimataifa kwa jina tu na havikidhi matakwa ya Fifa. Hii inaleta wasiwasi kuhusu dhamira ya serikali ya kuboresha miundombinu ya michezo nchini, alisema Namwamba.
Katika ziara yake katika Uwanja wa Masinde Muliro huko Kanduyi, Bungoma, Namwamba alitambua umuhimu wa kuwa na miundombinu ya michezo inayokidhi viwango vya kimataifa na vya Fifa. Alihakikishia wakazi wa Bungoma kwamba wanakandarasi wanaofanya kazi katika uwanja huo hawataacha mradi mpaka utakapokamilika na kuwa tayari kuandaa michezo ya CHAN.
Namwamba alisisitiza umuhimu wa kuwa na miundombinu bora ya michezo ili kuboresha shughuli za michezo nchini.
“Tunahitaji miundombinu bora ya michezo ili kuboresha shughuli za michezo yetu. Ninaahidi kuboresha miundombinu ya michezo nchi nzima kupitia serikali ya Kenya Kwanza,” alisema Ababu.
Aliangazia maendeleo ya ujenzi wa uwanja wa Masinde Muliro, akisema kuwa uko kwenye mkondo wa kukamilika kwa wakati ili kuandaa sherehe za Madaraka Day, Juni 1, 2024.
Licha ya changamoto zinazokabili miundombinu ya michezo nchini Kenya, Namwamba ana azma ya kuhakikisha miradi kama Uwanja wa Masinde Muliro inakamilika kwa viwango vya juu. Alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika mchakato wa ujenzi na kuwataka wanakandarasi kutilia mkazo ubora na kukamilika kwa wakati.