Michezo

Aiyabei avunja rekodi ya mbio za Frankfurt Marathon

October 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MKENYA Valary Aiyabei ndiye bingwa mpya wa Mbio za Mainova Frankfurt Marathon zilizoandaliwa Jumapili nchini Ujerumani.

Alifika utepeni baada ya muda wa saa 2:19:10 na kuvunja rekodi ya saa 2:20:36 iliyokuwa ikishikiliwa na raia wa Ethiopia Meskerem Assefa katika mbio hizo.

Ufanisi wa Aiyabei unamfanya kuwa mwanamke wa kwanza kuwahi kukamilisha mbio za Frankfurt Marathon kwa chini ya muda wa saa mbili na dakika 20.

Muda wa Aiyabei ndio wa tano wa kasi zaidi kuwahi kusajiliwa katika mbio za kilomita 42 msimu huu.

Aliwapiku raia wa Ethiopia Megertu Alemu (2:21:00) na Assefa (2:22:01) aliyepania kutetea ubingwa wake Jumapili.

Aiyabei ambaye hujiandalia katika eneo la Iten, Elgeyo Marakwet alichomoka katika kundi la wanariadha waliokuwa wakiongoza mbio hizo katika hatua za mapema.

Wanaume wa Kenya waliona giza katika mbio za Frankfurt Marathon na za Dublin City Marathon, Ireland mtawalia.

Fikre Tefera alitawala mbio za Frankfurt baada ya kusajili muda wa saa 2:07:08 mbele ya Mwethiopia mwenzake Dawit Wolde aliyeridhika na nafasi ya pili kwa muda wa saa 2:07:10. Aweke Ayalew wa Bahrain aliambulia nafasi ya tatu baada ya kusajili muda wa saa 2:07:12.

Kivumbi cha Dublin kilitamalakiwa na Othamane El Goumri wa Morocco aliyeweka rekodi mpya ya saa 2:08:07 katika mbio hizo. Stephen Scullion wa Jamhuri ya Ireland aliibuka wa pili kwa muda wa saa 2:12:01 mbele ya Mwethiopia Asefa Bekele aliyetawazwa mfalme wa mbio hizo mwaka 2018 kwa muda wa saa 2:13:24.

Dennis Kipkorir na Philemon Maritim waliowakilisha Kenya katika mbio hizo kwa upande wa wanaume waliambulia nafasi za saba na 16 mtawalia. Kipkorir alijibwaga ulingoni akijivunia muda bora wa dakika 30:24.52 alioutumia kuibuka na ushindi katika mbio za kilomita 10 jijini Kansas, Amerika mwaka huu.

Maritim alitumia muda wa saa 1:02:04 kukamilisha mbio za Prague Half Marathon nchini Czech mwanzoni mwa mwaka 2019.