• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
AK yafutilia mbali majaribio ya mbio kwa minajili ya kivumbi cha Kip Keino Classic

AK yafutilia mbali majaribio ya mbio kwa minajili ya kivumbi cha Kip Keino Classic

Na CHRIS ADUNGO

MAJARIBIO ya mbio za kujiandaa kwa Riadha za Kip Keino Classic yaliyokuwa yafanyike Jumapili ya Septemba 13 kabla ya kuahirishwa hadi Septemba 19, 2020 sasa yamefutiliwa mbali kabisa.

Kwa mujibu wa Paul Mutwii ambaye ni Naibu Rais wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK), shughuli za ukarabati katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi hazitakuwa zimekamilika kufikia siku ambapo majarabio ya mbio hizo yalikuwa yameratibiwa kufanyika.

AK ilipania kutumia majaribio hayo kuchuja baadhi ya wanariadha watakaowakilisha Kenya kwenye kivumbi cha Kip Keino Classic ambacho ni kati ya makala ya mbio za dunia za Continental Tour zitakazofanyika humu nchini mnamo Oktoba 3, 2020.

Mutwii ameshikilia kwamba AK isingehamishia mbio hizo za majaribio hadi uwanja wa MISC Kasarani kwa kuwa maazimio ya mchujo wenyewe yalikuwa ni kufanyia majaribio pia vifaa mbalimbali vitakavyotumiwa wakati wa Riadha za Kip Keino Classic.

“Ukarabati kwenye sehemu ya kukimbilia utaanza kesho Jumamosi ya Septemba 12. Hivyo, itakuwa vigumu sana kwa mashindano yoyote kuandaliwa ugani Nyayo kwa sasa. Septemba 19 itakuwa mapema sana,” akasema Mutwii.

Aidha, Mutwii amefichua kwamba AK imepunguza idadi ya wanariadha watakaonogesha kivumbi cha Kip Keino Classic kutoka 230 waliotazamiwa hadi 100 pekee kutokana na ushauri wa Wizara ya Afya katika juhudi za kukabiliana vilivyo na maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

“Wanariadha wote watakaoteuliwa kuwakilisha Kenya kwenye mbio hizo watafanyiwa vipimo vya corona kwa ada ya Sh5,000 kila mmoja kabla ya kupewa idhini ya kuingia kambini,” akatanguliza Mutwii.

“Hili ni zoeazi ghali ndiposa tumepunguza idadi zaidi. Watafanyiwa tena vipimo vingine saa 72 kabla ya kuanza mazoezi ya pamoja na hatimaye kushiriki kivumbi cha Kip Keino Classic,” akaongeza.

Mutwii amesema orodha ya watakaoshiriki mbio za Kip Keino Classic ambazo ni za mwisho kwenye msururu wa Riadha wa World Athletics Continental Tour, itatolewa na AK baadaye wiki ijayo.

Kwa mujibu wa Mutwii, washiriki watateuliwa kutokana na ubora wa fomu ya sasa, matokeo yao kwenye Riadha za Dunia za 2019 nchini Qatar na nafasi wanazozishikilia kwenye msimamo wa orodha ya viwango bora vya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).

“Kwa kuwa wengi wa wanariadha wetu bado hawajaingia katika orodha rasmi ya IAAF, kunao tutakaoteua kwa misingi ya matokeo yao ya kitaifa mwaka jana (iwapo walitinga tatu-bora kwenye fani zao) na jinsi walivyofaulu kwenye makala yaliyopita ya Riadha za Dunia,” akasema.

Mbio za Septemba 19 zililenga kuwapa vinara wa AK jukwaa la kufanyia majaribio vifaa mbalimbali katika uwanja wa Nyayo ambao umekuwa ukikarabatiwa tangu 2017.

Fani zitakazoshindaniwa kwenye Mbio za Kip Keino Classic ni kuruka mara tatu, urushaji wa kijiwe, mbio za mita 200, mita 3,000 kuruka viunzi na maji (wanaume na wanawake), urushaji mkuki (wanaume), mbio za mita 400, mita 800, mita 1,500 na mita 5,000 (wanaume na wanawake).

Fani nyinginezo ni matembezi ya kilomita 20, kuruka juu (wanaume), kuruka urefu (wanawake), mita 4×400 kupokezana vijiti, mita 400 kuruka viunzi na mita 10,000 (wanaume).

Kufikia sasa, duru tatu kati ya saba za Riadha za Continental Tour zimeandaliwa, ya hivi majuzi zaidi ikiwa ya Seiko Golden Grand Prix jijini Tokyo, Japan mnamo Agosti 22, 2020.

“Tuliona yaliyofanyika Finland, Hungary na Japan. Mbio za Continental Tour ziliendeshwa kwa utaratibu mzuri na mashabiki wakakubaliwa kuhudhuria. Hilo linatupa tumaini kubwa kwamba yawezekana pia kwa Kip Keino Classic kuandaliwa kwa namna hiyo,” akasema Mutwii.

  • Tags

You can share this post!

Tusker wamsajili beki wa haiba kutoka AFC Leopards

Yidah avunja ndoa na Sharks na kuyoyomea Nairobi City Stars