Michezo

AK yalenga kutafuta suluhu ya mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki

November 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) linapania kuandaa mchujo wa mbio za mita 10,000 miongoni mwa wanariadha watakaoshiriki Olimpiki za 2021 jijini Tokyo, Japan katika kipindi tofauti na fani nyinginezo.

Kwa mujibu wa kalenda mpya ya msimu wa 2021 iliyotolewa na mkurugenzi wa michezo wa AK Paul Mutwii mnamo Novemba 11, 2020, uteuzi wa kikosi kitakachopeperusha bendera ya Kenya nchini Japan katika mbio za mita 10,000 utafanywa mnamo Juni 26-27, 2021 jijini Nairobi.

Mchujo wa fani nyinginezo za mbio utaandaliwa jijini Nairobi kati ya Julai 2-3 jijini Nairobi.

Michezo ya Olimpiki ya Tokyo, Japan iliyokuwa ifanyike mnamo Julai 24 hadi Agosti 9 mwaka huu wa 2020 iliahirishwa kwa mwaka mmoja zaidi hadi Julai 23 mpaka Agosti 8, 2021 kwa sababu ya janga la corona.

“Tunapania kutafuta suluhu katika mbio za mita 10,000 na mita 5,000 baada ya nishani zote muhimu katika fani hiyo kutukwepa kwa kipindi kirefu kilichopita,” akasema Mutwii.

Mchujo wa kikosi kitakachowakilisha Kenya kwenye riadha za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 zitakazoandaliwa Julai 2021 umeratibiwa kufanyika Novemba 20-21 ugani Nyayo, Nairobi.

Kongamano la kila mwaka la AK ambalo huleta pamoja wanariadha wa sehemu mbalimbali za humu nchini linatarajiwa kuandaliwa jijini Nairobi mnamo Disemba 2-5, 2020. Kenya itatuma wanariadha kwenye mbio za kimataifa za ukumbini na za kupokezana vijiti mjini Silesia, Poland mnamo Mei 1-2, 2021.

 

Bingwa mara nne wa Olimpiki, Mo Farah, amethibitisha kwamba hatakuwa sehemu ya wanariadha watakaonogesha mbio za mita 5,000 kwenye Michezo ya Olimpiki itakayoandaliwa jijini Tokyo, Japan mnamo 2021.

Tangazo hilo la Farah linatazamiwa kuwapa Wakenya motisha zaidi ya kuzitamalaki mbio hizo.

Tangu mwaka wa 2005 ambapo Benjamin Limo alitawala mbio hizo katika Riadha za Dunia jijini Helsinki, Finland, Kenya haijawahi tena kunyakua medali ya dhahabu katika fani hiyo ambayo imekuwa ikitamalakiwa na Kenenisa Bekele wa Ethiopia na Mo Farah kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

Rekodi ya Kenya katika mbio hizo hata kwenye Michezo ya Olimpiki haijawa ya kuridhisha katika miaka 30 iliyopita.

John Ngugi ndiye Mkenya wa mwisho kuwahi kutia kapuni nishani ya dhahabu katika mbio hizo kwenye Olimpiki za Seoul, Korea Kusini mnamo 1988.

Farah, 37, aliibuka mshindi wa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 na mita 10,000 kwenye Olimpiki za London 2016 na Rio 2016 kabla ya kuelekeza makini yake kwenye mashindano ya marathon.

Hata hivyo, ameshikilia kwamba atalenga kuhifadhi ufalme wake kwenye mbio za mita 10,000 nchini Japan.

“Naendelea vizuri na maandalizi, ila nadhani muhimu zaidi ni kumakinikia fani moja na kuona ni nini ninachoweza kufanya,” akasema Farah.

Akitangaza marejeo yake kwenye mbio za masafa ya kadri, Farah alivunja rekodi ya dunia kwa kukimbia umbali wa mita 21,330 chini ya saa moja kwenye kivumbi cha Diamond League kilichoandaliwa jijini Brussels, Ubelgiji mnamo Septemba 4, 2020.

Baada ya ufanisi huo, alitawala Nusu Marathon ya Antrim Coast nchini Ireland ya Kaskazini mnamo Septemba 12 na akakaribia kuvunja rekodi yake mwenyewe kwenye mbio hizo za kilomita 21.