• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Akuei ni miongoni mwa wanaraga sita wa Kenya watakaonogesha IPL World 10’s Bermuda

Akuei ni miongoni mwa wanaraga sita wa Kenya watakaonogesha IPL World 10’s Bermuda

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI wa Kenya Simbas, Monate Akuei ni miongoni mwa wanaraga wa humu nchini ambao wameteuliwa kunogesha kipute cha dunia cha wanaraga 10 kila upande almaarufu ‘The IPL World Tens Series’ katika Kisiwa cha Bermuda mwezi huu wa Oktoba 2020.

Mbali na Akuei, wachezaji wengine wa humu nchini ambao wamealikwa kushiriki kivumbi hicho ni wanaraga watano wa timu ya taifa ya wachezaji saba kila upande, Shujaa. Hao ni pamoja na Andrew Amonde, Collins Injera, Willy Ambaka, Oscar Ouma na Oscar Dennis.

Akuei ameibukia kuwa mwanaraga tegemeo zaidi kambini mwa Simbas katika kipindi cha misimu miwili iliyopita baada ya kuridhisha sana akiwa mchezaji wa Nakuru RFC. Alikuwa pia sehemu ya kikosi cha Shujaa kilichoshiriki kampeni za Safari Sevens msimu uliopita wa 2019-20.

Mechi za kwanza za Akuei kuchezea Simbas ni zile zilizowakutanisha na Zambia na Zimbabwe kwenye Victoria Cup mnamo 2019.

Akuei amekuwa Amerika tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2020 na alitamba sana kwenye michuano ya duru ya Toger Serves Series mnamo Septemba 2020 kiasi cha kuwa kivutio cha waandalizi wa World Tens Series zitakazofanyika Bermuda.

Kwa kualikwa kushiriki kivumbi hicho, Akuei sasa atapata fursa ya kucheza pamoja na wanaraga maarufu zaidi katika vikosi vya wachezaji saba kila upande nchini Afrika Kusini, Fiji, New Zealand, Uingereza na Australia.

“Hiki kitakuwa kivumbi kikubwa. Tija na fahari zaidi ni kwamba nitacheza na baadhi ya wanaraga maarufu na wa haiba kubwa zaidi duniani,” akasema.

Kubwa zaidi katika matamanio ya Akuei ni kuona mchezo wa raga ukimsaidia siku moja kusafirisha familia yake kutoka Amerika na kurudi Kenya.

“Nalenga sana kusaidia familia yangu na pia kupata hifadhi kambini mwa kikosi kitakachonipa jukwaa zuri zaidi la kujikuza kitaaluma,” akaongeza kwa kusisitiza kwamba Kenya inajivunia idadi kubwa ya wanaraga walio na uwezo wa kuchezea vikosi mbalimbali vya New Zealand, Fiji, Amerika, Afrika Kusini na bara Ulaya.

Fowadi huyo anatazamia pia kuwa sehemu ya mechi kadhaa zijazo za Kenya Simbas, ikiwemo michuano ya kimataifa ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mnamo 2022.

Kufikia sasa wanaraga sita wa Kenya (Akuei, Amonde, Injera, Ambaka, Ouma na Dennis) watakuwa sehemu ya kikosi cha SFX 10 kutoka Cape Town, Afrika Kusini chini ya ukufunzi wa mwanaraga wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini almaarufu ‘Springbok Sevens’, Frankie Horne.

Nyota Cecil Afrika, 32, atakuwa miongoni mwa wanaraga watano wa ziada kutoka Afrika Kusini watakaoshirikiana na Wakenya katika kikosi cha SFX 10 – kampuni ya vyombo vya kielektroniki jijini Cape Town.

“Ni fahari tele kwamba wachezaji wa Kenya wamekubali kuwa sehemu ya kikosi chetu. Hawa ni wanaraga wa haiba kubwa wanaojivunia tajriba pevu kutokana na uzoefu wao kwenye raga ya kimataifa. Tumewateua kwa sababu Kenya ni mojawapo ya mataifa ambayo ni ngome ya wanaraga stadi barani Afrika,” akasema Horne katika taarifa yake kwa Shirikisho la Raga la Afrika Kusini (SARU) na kunukuliwa na gazeti la Daily Sun nchini Afrika Kusini.

Mechi za raundi ya kwanza ya kipute hicho Kisiwani Bermuda zitapigwa kati ya Oktoba 24-25 huku zile za raundi ya pili zikiandaliwa kati ya Oktoba 31 na Novemba 1. Michuano ya raundi ya mwisho (fainali) itasakatwa Novemba 7 uwanjani National Sports Centre, Bermuda.

Msururu wa mapambano hayo ya dunia ya wanaraga 10 kila upande yanashirikisha timu nane za wachezaji mahiri zaidi duniani wanaowakilisha watu binafsi, mashirika, asasi, taasisi au kampuni mbalimbali.

Wachezaji wote watakaoshiriki mechi hizo ndani ya viwanja vitupu wanatakiwa kufanyiwa vipimo vya corona kufikia Oktoba 15, 2020.

  • Tags

You can share this post!

Ruiru, mtaa unaokua kwa kasi kufuatia kujengwa kwa Thika...

Ireland sasa yaita Maguire na Horgan kuokoa jahazi