Michezo

Al Swafaa na Waterworks wawania ubabe

May 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

MICHEZO ya kuwania taji la Nairobi West Regional League (NWRL) kwa wanaume iliendelea kutokota huku Al Swafaa FC na Waterworks kila moja ikijiongezea alama nne na kuendelea kukabana koo.

Wachezaji wa Al Swafaa walitoka nguvu sawa mabao 2-2 na Kibera Saints kisha walikomoa Dagoretti Lions mabao 4-2. Nayo Waterworks ilinyanyua Riruta United (Makarios 111) magoli 3-0 baadaye ililazimishwa kuagana sare ya bao 1-1 na Nairobi Prisons.

Licha ya matokeo hayo Al Swafaa ingali kifua mbele kwa alama 24 sawa na Waterworks tofauti ikiwa idadi ya mabao.

”Tumebakisha mechi mbili pekee ili kukamilisha ratiba ya msimu huu ambapo wapinzani wote wanapiga gozi ya ng’ombe kama fainali ya pesa ndefu,” kocha wa Al Swafaa, Charles ‘Stam’ Kaindi alisema.

Ufanisi wa Al Swafaa ulipatikana kupitia Abdul Abubakar, James Malwar, Fredrick Juma na Edward Mungai aliyeibuka mchezaji nyota kwenye mechi hiyo. Waliofungia Waterworks walikuwa Masha Kalume, Enock Momanyi, Zumberi Mohammed pia Oscar Iwajika.

”Al Swafaa imekaa pazuri kunasa tiketi hiyo maana mwanzo itacheza na Nairobi Prisons kisha itakuja kwetu kwenye patashika ya mwisho,” kocha wa Waterworks, Anthony Nderitu alisema. Timu itakayobeba ubingwa huo moja kwa moja itafuzu kupandishwa ngazi kushiriki mechi za Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu ujao.

Kwenye matokeo mengine kundi hilo, Kibera Saints ilituzwa alama tatu bila jasho baada ya Real Mathare kuingia mitini.

Kwenye mechi za Kundi B kipute hicho, Makombora bulls ilipigwa mabao 2-0 na WYSA na AFC Leopards ililazwa mabao 4-3 na KEMRI.