Michezo

Al Swafaa waibuka washindi wa Ramadhan Cup

June 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

Al Swafaa FC ilitawazwa mabingwa wa shindano la Ramadhan Cup 2019 baada ya kulaza Kibera Soccer mabao 3-1 kupitia mikwanju ya penalti katika fainali iliyopigiwa uwanjani Woodley Kibera, Nairobi.

Al Swafaa ya kocha, Charles ‘Stam’ Kaindi ilitwaa ubingwa huo licha ya kuonekana kulemewa na wapinzani wao kwenye mechi hiyo iliyomalizika sare tasa katika muda wa kawaida.

Waliofungia Al Swafaa walikuwa Abdallah Mohammed, Antony Munene na Paul Odera nalo bao la Kibera Soccer lilifumwa na Ammar Munawar.

Akipongeza wachezaji wa Al Swafaa FC, mwenyekiti wa Shirikisho la Soka ya Kenya (FKF) Tawi la Nairobi Magharibi, Hussein Bashir alisema “Shindano hili huandaliwa kila mwaka wakati wa mfungo wa ramadhan ili kuleta vijana pamoja pia kukuza talanta za wachezaji chipukizi mtaani.”

Kocha Charles ‘Stam’ Kaindi wa Al Swafaa FC akituzwa baada ya kikosi hicho kutawazwa mabingwa Radhaman Cup 2019 uwanjani Woodley Kibera, Nairobi. Picha/ John Kimwere

Pia alishukuru shirika la GoTV ambalo limekuwa mfadhili wa shindano hilo kwa muda sasa. Kadhalika alipongeza timu zote zilizoshiriki kipute hicho licha ya changamoto za hapa na pale maana nyakati zingine mvua ilikuwa inakatiza mechi vijana wakiwa uwanjani.

Nayo timu ya Mashujaa iliibuka ya tatu kwa kutuzwa ushindi wa mezani baada ya Gogo Boys kuingia mitini. GoTV ilitoa zawadi tofauti ikiwamo pesa taslimu kwa timu tatu za kwanza pia wachezaji waliofana kwenye shindano hilo.

Al Swafaa ilitwaa tikiti ya fainali iliponyanyua Gogo Boys mabao 5-4 kupitia mikwanju ya penalti baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwenye nusu fainali ya kwanza. Kwenye nusu fainali ya pili Kibera Soccer ilifanya kweli ilizoa ufanisi wa mabao 4-1 mbele ya Mashujaa FC.