Alan Shearer: Mtarajie mabadiliko juu ya jedwali la EPL Jumatano usiku
MWANASOKA mstaafu, Alan Shearer amesema ingawa Liverpool wako uongozini mwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa pointi 67, mbele ya Arsenal walio na 65, hakuna atakayezuia Manchester City kuhifadhi taji hilo.
Manchester City inakamata nafasi ya tatu ikiwa na 64, huku ikijivunia rekodi ya kutoshindwa katika mechi 23 katika mashindano tofauti, lakini jagina huyo amesema hisia zake hazitegemei kiwango cha sasa cha kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola.
Baadhi ya matokeo yao katika mechi zilizopita sio ya kuridhisha, ikiwemo sare ya 0-0 dhidi ya Arsenal katika mechi ya EPL iliyochezewa Etihad, Jumapili.
Shearer amesema anatarajia msimu kubadilika wakati City wataalika Aston Villa leo usiku ugani Etihad, mechi ambayo anaamini wenyeji watashinda.
Alisema nguvu yao, ni pamoja na kuandikisha matokeo katika mechi muhimu, kama iliyopita baada ya kucheza vibaya.
Matokeo ya sare katika mechi ya wikendi yalikuwa muhimu kwa Arsenal ambao walitarajiwa kuchapwa wakati huu City wamebakisha mechi tisa kukamilisha ratiba ya 2023/2024.
“Nilibashiri wataibuka washindi hata kabla ya msimu kuanza, na bado nafikiria hivyo, ingawa walicheza kwa kiwango cha chini Jumapili, kinyume na walivyocheza miezi 11 iliyopita katika mechi ambayo walicharaza Arsenal 4-1 katika safari yao ya kuwania ubingwa.
Jumapili, Arsenal walionyesha mabadliko makubwa hasa baada ya kupata wachezaji kadhaa wapya akiwemo Declan Rice ambaye ameleta mabadiliko makubwa katika safu yao ya kiungo.
Shearer alisema itakuwa vigumu kwa timu yeyote kupata ushindi ugani Etihad ambako City wamefunga mabao 47 mfululizo.
“Itakuwa vigumu kwa timu yeyote kupata ushindi katika uwanja huo wao wa nyumbani. Arsenal walipata nafasi kadhaa, lakini Gabriel Jesus na Leandro Trossard wakashindwa kufunga. Ni mechi ambayo mpango wa Arsenal ulifaulu na wakaondoka na pointi moja, lakini wangeshinda kama wangetumia nafasi zao vizuri.”
City walifunga mabao mengi hapo awali kabla ya mapumziko ya wiki mbili kwa ajili ya mechi kimataifa, na bila shaka wataamka tena na kuanza kuwa moto wa kuotea mbali katika mechi za nyumbani.
Kwa jumla, Arsenal waliponea. Watu watarajie mabadiliko kwenye msimamo wa EPL kuanzia kesho, Jumatano usiku.”
“Nimeangalia mechi zilizobakia na kuona za City zikiwa nafuu ikilinganishwa na wapinzani wao wa karibu. Kwa sasa, kikosi cha Jurgen Klopp hakivutii kama ilivyotarajiwa kutokana na majeraha ya mara kwa mara kwa baadhi ya wachezaji wake muhimu, hivyo, wataendelea kupata matokeo ya kuchanganya.”
Klopp anategemea wachezaji fulani kushinda mechi. Wachezaji hao ni pamoja na Mohamed Salah ambaye kiwango chake kimeshuka kwa sasa.
Ingawa ni miongoni mwa waliofunga dhidi ya Brighton, amekuwa akipoteza nafasi nyingi hata akiwa karibu na lango. Katika mechi iliyopita, Salah alipoteza nafasi nyingi kabla ya kufunga bao katika ushindi wao wa 2-1,” aliongeza Shearer.