Michezo

Alenga kuisaidia Coast Stima ishiriki kipute cha KPL

May 10th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KILA mchezaji wa soka huwa na hamu afikie kiwango cha kuchezea Ligi Kuu ya nchi yake pamoja na timu yake ya taifa.

Kwake mchezaji Khamis Abud hakukuwa na tofauti kwani alikuwa na hamu ya kuichezea timu ya Bandari FC inayoshiriki kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL), lakini ndoto yake hiyo haikufanikiwa kutokana na timu hiyo kutompa nafasi ya kuonyesha ubora wake mwaka 2016.

Abud, 25, alikuwa amesajiliwa na Bandari msimu huo wa 2016 kutoka Uweza FC iliyokuwa ikishiriki Ligi ya Kaunti ya Nairobi, lakini alipokosa kupewa nafasi, aliamua kujiunga na Coast Stima FC inayoshiriki Supa Ligi ya Taifa mwaka 2017.

“Nina furaha kuichezea Stima kwani nina imani kubwa hatuko mbali kupanda ngazi hadi KPL. Tuna kikosi ambacho ninaamini kinaweza kufanya vizuri na kuangazia kuwa timu ya pili ya Pwani kuwa katika ligi kuu,” anasema Abud.

Kama walivyochipuka wanasoka wengi wazuri kutoka mtaa wa Majengo ambao ni kama vile wana vipaji vya kuzaliwa vya kusakata soka, Abud alionekana kuwa mchezaji mzuri alipokwenda kumtembelea shangazi yake jijini Nairobi ambapo alivutia timu ya mtaa wa Kibera ya Uweza FC.

“Kujiunga kwangu na Uweza mwaka 2014 kulikuwa ndio mwanzo wa safari yangu ya kuelekea mbali na hasa ndoto yangu ya kuchezea klabu yoyote ya ligi kuu ya kwetu Pwani na kwa kuwa timu ilikuwa Bandari FC, nilifurahi waliponishuhudia huko Nairobi na wakanisajili,” anasema.

Abud alifanya bidii ya mazoezi katika timu hiyo ya Bandari lakini hakupata fursa ya kucheza ila kuwa mchezaji wa akiba na alipoona hana tumaini la kuchezeshwa, aliamua kuihama na kujiunga na Coast Stima FC ambayo angali anaichezea.

Akiwa mchezaji anayechezea nafasi ya winga, Abud anaamini baadhi ya wanasoka wengine kutoka Bandari kina Hassan Idd na Dennis Magige ambao nao pia wamejiunga na Stima, wana uwezo na bila shaka “watafika mbali.”

“Tumepania msimu huu kumaliza msimu huu katika Top 3 lakini kutokana na kuvunjwa kwa ligi kwa sababu ya tatizo la ugonjwa wa corona, nina imani msimu ujao tunaweza kushinda taji la Supaligi la msimu wa 2020-2021,” akasema Abud.

Mbali na kutaka kufika na kukipiga katika ligi kuu, Abud ambaye ni shabiki sugu wa timu ya Juventus FC ya Italia na anayejaribu kuiga mbinu za uchezaji wa Ronaldo, ameazimia kufanya bidii hadi kucheza soka la kulipwa huko barani Ulaya.

Mchezaji wa klabu ya Coast Stima FC Khamis Abud (kati). Picha/ Abdulrahman Sheriff

“Kiuhakika, ningependa nikifikia kiwango cha kucheza soka la kulipwa, nichezee ama Juventus ya Italia au Arsenal ya Uingereza lakini kama si hizo basi timu yoyote ile itakayotaka kunisajili,” anasema mwanasoka huyo.

Anamsifu mkufunzi wake Athman Juma almaarufu Rila kwa jinsi alivyojitahidi na anazidi kuinua vipaji vya wanasoka wengi wa Majengo wakiwemo Ali Abubakar aliyesajiliwa na Bandari Youth, Alfred Maningi anayechezea Coast Stima na Hashim Ali aliyeko Qatar.

Abud anawasihi wanasoka wenzake wa Majengo na wa Pwani kwa jumla kuwa ni bidii ya mazoezi na nidhamu ndivyo vyombo vikuu ambavyo vinaweza kumfanya mchezaji atambulike na kuinua vipaji vya uchezaji wake.

“Bidii ya mazoezi na kuwa na nidhamu ya hali ya juu kunamsaidia mwanasoka kuinua kipaji chake kwa haraka. Hivyo, nawaomba wenzangu wa Pwani wawe wenye kutekeleza hayo ili wapande na kuwa wanasoka wa kutambulika nchini na ng’ambo,” anasema.

Anasema wamepania yeye pamoja na wenzake katika klabu yake hiyo ya Coast Stima kuhakikisha wanashinda mechi zao zilizobakia za msimu huu lakini wanaangazia zaidi kuhakikisha wanashinda ligi hiyo na kushiriki ligi kuu msimu wa 2021-2022.