ALEX ADUVAGA: Akikulisha kadi nyekundu, bila shaka ulimlazimisha
Na PATRICK KILAVUKA
Mkondo wa maisha hurithiwa, huigwa au huwa neema ya Maulana kwani yeye ndiye mpaji na mwanzilishi wa kila kitu.
Hivyo ndiyo anavyoamini refa Alex Kenyani Aduvaga ambaye sifa zake za kufanya maamuzi ya kabumbu uwanjani huwawaachi mashabiki na wadau wa vilabu wakitamauka kwani, huwa anatumia jicho lake pevu kusawazisha mambo ugani na kudhibiti dhoruba za mchezo hadi mwisho mwa gemu.
Anasema akiwa kinda, alikuwa anapenda kukimbia akipuliza firimbi huku akiwa na saa ya mkono pasi na kujua kwamba, anapanda mbegu ya kuwa refa japo aliuchukulia kama uraibu tu hadi sasa ambapo anang’amua kwamba mambo mengine ni utajiri wa usoni.
Mwamuzi huyu anajulikana kwa utani “mrefu au tall” kutokana na urefa wake wa kima cha mita 6.9. Anadokeza kwamba, akiwa uwanjani mawazo yake huwa ameyaweka kwa shughuli mzima ya mchezo.
“Ninaamini kwamba, nikiwa uwanjani mimi muamuzi. Ninafaa kuusimamia mchuano kwa njia isiyokuwa na bughudha yeyote kwani macho yote yako kwangu wakati niposukuma gurudumu hilo la dakika tisini au zaidi,” asema refa huyo ambaye hana masihara uwanjani kwa mchezaji wowote ambaye analeta kichefuchefu uwanjani au achezaye ndiyo sivyo.
Hata hivyo, anasema hakuzaliwa akiwa muamuzi wa kandanda bali safari yake ilitanuka baada ya kushawishiwa na muamuzi kigogo na anayesimamia marefa wa tawi la Nairobi West katika Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF) Bw Aggrey Shavera kujitosa katika kazi hii. Akiwa shuleni, alikuwa mwanasoka hodari.
“Nilisomea na kuchezea Shule ya Msingi na Sekondari ya Mbihi, Kaunti ya Vihiga Kabla kujiunga na timu ya Brookside FC 1992-1999. Hatimaye, niliichezea Mbihi Rangers 1999-2000 kabla kuhamia Nairobi,” asema refa Kenyani ambaye alikuwa anachezea kama winga wa kushoto. Kando na hayo, anaichezea timu ya marefa ya Westlands.
Mpuliza firimbi huyu anasema alipotua jijini Nairobi, nia ilikuwa atafute riziki kwanza. Alipatana na msamaria mwema kwa jina Kapila Mugo ambaye alimweka katika barabara tofuati na kile alichopenda kandanda kwa kumpatia mshawasha wa kujituma kujifunza kazi ya useremala.
“Nilifunzwa kwa miezi minane na nikajua,” anasema refa-seremala Kenyani ambaye huunda fanicha za kutamanika kabla kuyoyomea viwanjani.
Baada ya kupata maarifa ya useremala, aliweza kufanya kazi hiyo na kampuni ya Cables na Kingpost hadi mwaka 2011 alipozama kabisa katika mambo ya urefa baada ya kusomea kazi hiyo.
“Mrefu” anasema ilikuwa baada ya kuchezesha mchuano wa Leviticus FC dhidi ya WYSA ndiposa refa Shavera alimsihi amshike mkono.
“Baada ya kuona vile nilichezesha mechi hiyo ya kirafiki kwa weledi mithili ya kupokea mafunzo maalum, alinielekeza hadi nikapokea mafunzo ya urefa na baada ya kumaliza nikaanza kupata fursa ya kuchezesha gemu nyingine nyingi,” anadokeza muamuzi wa kandanda huyo ambaye huchezesha michuano za Shirikisho la Kandanda Nchini – FKF (zamani KFF), mashindano ya shule za msingi, upili, vyuo na vyuo vikuu pamoja na vipute mbalimbali.
Katika daraja ya FKF, alianza kuchezesha mechi za Kauntindogo, Kaunti, Kanda( Regional) mwaka 2010 -2013 kabla kupandishwa ngazi kuchezesha Daraja ya Pili ambapo amezuru sehemu mbalimbali za Kaunti ya Nairobi na Kiambu kuchezesha.
Kati ya mechi za Divisheni ya Pili ambazo amewahi kuzichezesha huku ushindani ukiwa mkali ni zile zilikutanisha Limuru Olympic na Muranga Seal kwenye fainali ambapo Olympic iliinyuka Seal 2-0, Muranga Seal dhidi ya Karatina -mshindi akawa Seal baada ya kuichapa Karatina 2-1 na Gathanga dhidi ya Gatongora ambapo Gathanga waliponyoka na ushindi wa 2-1.
Kando na hizo, mechi ambazo zilikuwa zenye mawimbi makali ya soka ingawa alimudu kuyathibiti ni ile ya FKF, Daraja ya Pili, kati ya PCEA Kikuyu na Magana uwanjani KARI, Kikuyu na Lopez dhidi ya Tandaza uwanja wa Chuo cha Kikuu cha Lower Kabete.
“Nilithibiti presha kutoka pande zote kwa kuiyeyusha na tajriba yangu ya kazi ya urefa,” anakiri “Mrefu”.
Aghalabu, amechezesha Michezo ya Shirikisho la Shule za Upili Nchini, Nairobi na ya Vyuo Vikuu Nchini KUSA, Kanda ya Nairobi ambapo amechezesha kwa miaka Minne mtawalia. Pia, amewahi kuwa maamuzi wa Ligi ya Soka ya Vyuo Vikuu na Anuwai (UCFL) miaka mitatu 2016-2018.
Katika vipute, amechezesha kile cha Tim Wanyonyi Super Cup kaunti ndogo ya Westlands tangu kuanzishwa. Mwaka jana, alitawazwa refa bora wa mwaka 2018.
Isitoshe, alichezesha fainali za Chapa Dimba mwaka jana eneo la Nairobi na Gor Mahia Youth wakaibuka mabingwa baada ya kuchabanga JMJ Academy 3-0 ugani Stima Club.
Kazi ya urefa kwake anasema imekuwa rahisi kutokana na yeye kujituma kujinoa na kuzingatia sheria za kabumbu.
“Ninahakisha ninafanya mazoezi kila asubuhi Jumatatu hadi Alhamisi na Ijumaa jioni. Isitoshe, ninafanya mazoezi ya kifungua viungo ya Yoga kila Jumanne na Ijumaa saa tatu -saa nne,” anasema refa huyo na kusisitiza kwamba, mazoezi hayo makali yanamwezesha kupigisha michuano mengi pasipo kuchoka.
Anawianishaje kazi ya useremala na urefa? Kwanza kabisa, anasema anaipenda kazi ya urefa kama chanda na pete na anaifurahia. Hata hivyo, lisilobudi hutendewa.
Yeye hushughulikia kazi ya mbao kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa na urefa wikendi kunyeshe kusinyeshe! Anaongezea kwamba, endapo kazi ya urefa inaibuka katikati mwa Juma, yeye huwa radhi kuifanya.
Marefa chipukizi ambao amewashika mkono na kuwahimiza kujitosa katika kazi hii ni Brian Mudegu, Mwangi Kimani na Daniel Liyai.
Angependa kuchezesha soka hadi afikie kiwango cha refa wa Fifa Webb ambaye alichezesha fainali za Kombe la Dunia na Mpuliza kipenga Mike Din ambaye anachezesha Ligi ya Uingereza.
Mafanikio ambayo ameyapata kama refa ni kwamba, imekuwa kazi au njia ya kujitafutia riziki. Amezama katika kuzijua sheria zote kumi na saba za urefa akilenga kuinuliwa. Ametalii na kutangamana na watu wa tabaka mbalimbali wakiwemo wachezaji na mashabiki.
“Kutokana na mtagusano na watu wa kila hulka umechangia mimi kushikilia mikoba ya urefa sawasawa na hata kutambuliwa kama refa bora katika kipute alichokitaja,” anadokeza refa Mrefu.
Changamoto ambazo amekutana nazo katika safari yake ya Uamuzi wa gemu ni presha za makocha na wachezaji, visa vya utovu wa nidhamu miongoni mwa mashabiki na wachezaji, kejeli za kila aina ukiwa haswa refa wa kati.
Ushauri wake ni kwamba, urefa ni kazi yenye changamoto lakini unafaa kuzichukulia kama njia ya kuhimiza utangamano na watu wa hulka, tabia na uraibu mbalimbali. Chipukizi wa kila jinsia wafaa kujitokeza kujifunza.