• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Alex Song aliyewahi kutamba Arsenal na Barcelona asajiliwa na kikosi cha Arta/Solar7 nchini Djibouti

Alex Song aliyewahi kutamba Arsenal na Barcelona asajiliwa na kikosi cha Arta/Solar7 nchini Djibouti

Na MASHIRIKA

KIUNGO wa zamani wa Arsenal na Barcelona, Alex Song, 33, amejiunga rasmi na kikosi cha Arta/Solar7 kinachoshiriki Ligi Kuu ya Djibouti.

Nyota huyo raia wa Cameroon amerasimisha uhamisho wake hadi Arta kwa kutia saini mkataba wa miaka miwili. Song anajiunga na Arta miezi minane baada ya kubanduka kambini mwa FC Sion ya Ligi Kuu ya Uswisi.

Mnamo Machi 2020, kikosi cha FC Sion kiliwapiga kalamu wachezaji tisa waliokataa kutia saini makubaliano ya kupunguziwa mshahara baada ya mlipuko wa corona kutikisa uthabiti wa klabu hiyo kifedha.

Nyota wawili wa zamani wa Arsenal – Song na Johan Djourou ni miongoni mwa masogora hao waliotakiwa kuondoka kambini mwa Sion mwishoni mwa mwezi Machi. Wachezaji wengine walikuwa nahodha Xavier Kouassi, nyota wa zamani wa Newcastle United Seydou Doumbia, Ermir Lenjani, Mickael Facchinetti, Christian Zock, Birama Ndoye na aliyekuwa kiungo wa Fulham, Pajtim Kasami.

Ligi Kuu ya Uswisi ilisitishwa rasmi mnamo Machi 1 baada ya serikali ya taifa hilo kupiga marufuku mikutano ya hadhara inayohusisha zaidi ya watu 1,000 kwa wakati mmoja.

Kwa mujibu wa mtandao wa Football237 ambao umenukuliwa na gazeti la L’Equipe, Song kwa sasa atakuwa akichezea Arta na pia kusimamia makuzi na maendeleo ya chipukizi wa kikosi hicho kisoka.

Arta ambao walitawazwa mabingwa wa taji la Djibouti Cup mnamo 2020, wanatarajiwa kunogesha kivumbi cha kimataifa cha Kombe la Mashirikisho barani Afrika (Caf Confederation Cup) msimu huu.

Mnamo Oktoba 2020, Song alitangaza kwamba alikuwa amekamilisha kujenga shule kubwa jijini Douala ambayo itakuwa na vitengo vya wanafunzi wa chekechea, msingi na upili.

Mbali na kuchezea Arsenal, Barcelona na Sion, Song anajivunia pia kuvalia jezi za vikosi kadhaa barani Ulaya vikiwemo Bastia, Charlton Athletic, Barcelona, West Ham United na Rubin Kazan.

Miezi michache iliyopita, Song alikiri kwamba maamuzi yake ya kubanduka Arsenal na kutua Barcelona mnamo 2012 yalichochewa pakubwa na unono wa ofa aliyopokezwa na miamba hao wa soka ya Uhispania.

“Nilionywa sana kwamba nisingepata muda wa kutosha kuunga kikosi cha kwanza cha Barcelona. Nilivutiwa zaidi na wingi wa fedha ambazo ningekuwa nikipokea. Sikuwa na muda wa kuwaza zaidi,” akatanguliza.

“Nilitamani sana nipate fedha nyingi ndipo mke wangu na watoto wafurahie maisha. Nilikutana na mkurugenzi wa michezo kambini mwa Arsenal ambaye alinikataza kutua Barcelona na kuonya kwamba hatua hiyo ingesambaratisha taaluma yangu. Nilikaidi kwa sababu nilihisi ananinyima fursa ya kuwa milionea,” akasema Song akihojiwa na gazeti la L’Equipe.

Kariobangi Sharks ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) iliwahi kukutana na Arta/Solar7 ya Djibouti kwenye soka ya Caf Confederation Cup mnamo Novemba 2018 na kuwapokeza kichapo cha 6-1 uwanjani MISC Kasarani katika mkondo wa kwanza kabla ya kusajili ushindi wa 3-1 kwenye marudiano yaliyofanyika Djibouti mnamo Disemba 5, 2018.

You can share this post!

Pigo Northern Ireland baada ya mwanasoka tegemeo Corry...

Kenya hatarini kunyimwa mikopo kufuatia deni la Sh7 trilioni