Aliyekuwa kiungo wa Gor asajiliwa kuipandisha Shabana kwa KPL
NA CECIL ODONGO
KIUNGO wa zamani wa Gor Mahia Moses Otieno amejiunga na washiriki wapya wa ligi ya kitaifa ya Supa (NSL), Shabana FC ili kuwasakatia msimu wa 2018-19 timu hiyo inapolenga kukea ngazi kujiunga na ligi kuu nchini KPL.
“Tumekamilisha usajili wa Moses Otieno, kiungo mwenye kipaji cha ajabu. Huduma zake faafu zitatuwezesha kung’aa katika ligi ya Supa na mashindano mengine. Kwa kuwa ni mchezaji ambaye husakata soka ya kuvutia tunaamini atutuvumisha vilivyo kwenye mechi zetu,” ikasema taarifa kwenye mtandao wa Shabana FC.
Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 34 anakumbukwa sana kutokana na kung’aa kwake akisakatia Gor Mahia na pia kuvuma sana akiwa kwenye kikosi cha timu ya taifa Harambee Stars.
Kando na kuwajibikia K’Ogalo, Otieno ambaye alikuwa mwanafunzi wa zamani wa Kakamega High, shule inayotambulika kwa kutwaa mataji mengi ya soka nchini vile vile amewahi kuwatandazia Nakumatt FC, City Stars, Posta Rangers FC na Tusker.
Shabana, walijahakikishia nafasi katika NSL baada ya kuibuka wa pili katika ligi ya daraja ya tatu zoni B kisha kushinda mechi ya mchujo kupitia mikwaju ya penalti dhidi ya Mwatate FC kutoka kauti ya Taita Taveta ugani MISC Kasarani mwezi Oktoba.