Aliyekuwa kocha wa Brighton asema hakutarajia angepigwa kalamu
NA CECIL ODONGO
ALIYEKUWA Mkufunzi wa Brighton Chris Hughton amesema alishangazwa na hatua ya uongozi wa klabu hiyo kumtimua kama kocha wa timu hiyo.
Hughton aliye na umri wa miaka 60, alifutwa kazi Mei 13 kutokana na matokeo mabaya ya Brighton walioponyoka kuteremshwa ngazi kwa alama mbili pekee.
Kupitia taarifa aliyoandikia Muungano Simamizi wa Ligi Kuu ya Uingereza(EPL), mkufunzi huyo alilalamika kwamba uamuzi huo ulichukuliwa kwa pupa wala hakuarifiwa mapema kwamba angemwaga unga mwishoni mwa msimu wa 2018/19.
“Nilishtushwa na kughadhabishwa na uamuzi ulionipokonya kazi yangu kama mkufunzi wa Brighton and Hove Albion FC. Hata hivyo ningependa kuwashukuru wakufunzi wenzangu timuni, wachezaji na kila mtu ndani ya klabu aliyefanya kazi nami kuyaboresha matokeo ya timu,” akasema Hughton.
“Ingawa nalalamika, ningependa kusema nilifurahia muda wa miaka minne na nusu nilioifunza Brighton. Sina kinyongo na mtu ila sielewi kwa nini nilitimuliwa na kutimuliwa huko pia kulifanywa kwa njia isiyofaa,” akaongeza Hughton.
Brighton Jumanne Mei 21, 2019 ilimteua kocha wa zamani wa Swansea City Graham Potter kama mkufunzi wao na akamwaga wino kwenye kandarasi itakayomweka ugani American Express Community hadi 2023