• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
Amiens waanza mchakato wa kisheria kupinga hatua ya kushushwa ngazi Ligue 1

Amiens waanza mchakato wa kisheria kupinga hatua ya kushushwa ngazi Ligue 1

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

KIKOSI cha Amiens nchini Ufaransa kimeanza mchakato wa kisheria dhidi ya “maonevu” baada ya kuteremshwa ngazi kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) msimu huu.

Maamuzi hayo yaliyoshuhudia Amiens na Toulouse wakishushwa daraja huku Paris Saint-Germain (PSG) wakitawazwa mabingwa wa Ligue 1 yalichochewa na hatua ya msimu wa soka ya Ufaransa ukifutiliwa mbali kutokana na janga la corona.

Hadi hatua hiyo ilipochukuliwa, Amiens walikuwa wakishikilia nafasi ya 19 jedwalini kwa alama nne zaidi nyuma ya Nimes huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na Toulouse waliokuwa wakikokota nanga mkiani zikisalia mechi 10 pekee kwa kampeni za muhula huu kutamatika rasmi.

“Tutapigana kadri ya uwezo wetu kupinga maamuzi ya kibaguzi ambayo hayaonyeshi sifa nzuri za uanaspoti. Kwa hakika, maamuzi hayo ni sawa na adhabu kwa Amiens. Si haki, si sawa,” akasema Mwenyekiti wa Amiens, Bernard Joannin.

Kwa upande wake, wakili wa Amiens Christophe Bertrand alisema, “hatupingi kabisa maamuzi yaliyochukuliwa na wasimamizi wa soka ya Ufaransa kwa ushirikiano na serikali. Tunachopinga katika wasilisho letu rasmi kortini ni matokeo ya maamuzi hayo kwa mustakabali wa kikosi cha Amiens.”

Mwanzoni mwa mwezi huu, Amiens waliwasilisha kesi ya kudai haki kutoka kwa Shirikisho la Soka la Ufaransa baada ya kushushwa ngazi kwenye Ligue 1 na nafasi yao na Toulouse kutwaliwa na Lorient na Lens waliopandishwa ngazi kutoka Ligi ya Daraja la Kwanza (Ligue 2).

PSG sasa watashiriki kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao kwa pamoja na Marseille na Rennes waliofunga orodha ya vikosi vitatu-bora kileleni. Lille waliokamata nafasi ya nne watanogesha kipute cha Europa League.

Amiens wanawataka kubatilishwa kwa maamuzi ya kushusha ngazi vikosi viwili kwenye Ligue 1 na badala yake kudumisha klabu zote zilizoshiriki kivumbi hicho muhula huu kisha kujumuishwa kwa Lorient na Lens ili kipute cha Ligue 1 msimu ujao wa 2020-21 kiwe na jumla ya timu 22 badala ya 20.

You can share this post!

Nalenga kuvunja dhana potovu ‘Wakenya hawana lao soka...

COVID-19: Muuguzi Sarah Mosop yuko mstari wa mbele...

adminleo