Michezo

Amina amdengua Apew mashindano ya Afrika

March 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES ONGADI 

MATUMAINI ya Kenya kushinda medali katika mchezo wa ndondi katika Mashindano ya Afrika yanayoendelea Accra nchini Ghana yaliongezeka baada ya ushindi wa Amina Martha Faki.

Bondia Amina alirudisha matumaini ya Wakenya katika Mashindano haya baada ya kumkomoa Sarah Apew wa Ghana kwa pointi 5-0.

Licha kuzichapa mbele ya mashabiki wa nyumbani, Apew alishindwa kuhimili mashambulizi makali kutoka kwa Amina aliyechanganya ngumi za kushoto na kulia zilizomfanya kupepesuka kila mara ulingoni.

Katika pigano hilo la uzani wa Bantam, Amina alihakikisha amemweka mpinzani wake karibu huku akiwachilia mangumi ya kichwa, tumbo na kifua kila mara.

Ushindi wa Amina unakuja siku moja baada ya Peter Abuti Alwanga kupoteza pigano lake la ufunguzi dhidi ya Adams Olaore wa Nigeria katika uzani wa Heavy na kuweka Kenya katika hali ya mchecheto.

Aidha, bondia Aloice Ochieng’ Vincent anayewakilisha taifa kwa mara ya kwanza, anatarajiwa kupanda ulingoni leo, Jumapili, Machi 17, 2024 kupepetana na Mbaya Mulumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika uzani wa Lightwelter.

Bondia mwingine wa Kenya anayetarajiwa kucheza ni Edwin Okong’o katika uzani wa Middle na anayechezea klabu ya Jeshi (KDF) katika ligi kuu nchini.

Mashindano haya yamevutia mabondia 212, wakiwemo 148 wa kiume na 64 wa kike kutoka mataifa 33.