Michezo

Ancelotti ashtakiwa kukwepa kulipa ushuru akiwa Real

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Carlo Ancelotti wa Everton ameshtakiwa nchini Uhispania kwa hatia ya kutolipa ushuru wa hadi Sh127 milioni alipokuwa mkufunzi wa Real Madrid.

Kwa mujibu wa stakabadhi za waendeshaji wa mashatka nchini Uhispania, Ancelotti mwenye umri wa miaka 61 alikataa kufichua kiwango cha mapata yake katika kipindi kizima cha kuhudumu kwake katika soka ya Uhispania kwa nia ya kuhepa kutozwa ushuru.

Ancelotti alikuwa atozwe kiwango hicho cha ushuru kutoka kwa fedha alizopokezwa kutokana na mapato ya haki ya matumizi ya picha zake kwa kipindi cha msimu wa 2013-15 alipokuwa akidhibiti mikoba ya Real Madrid. Katika taarifa yao, Everton wamesema kwamba hawawezi kulizungumzia suala hilo kwa sasa.

Ancelotti si mtu wa kwanza kuwahi kushtakiwa kwa hatia ya kuhepa kulipa ushuru nchini Uhispania. Wanasoka wengine wa haiba kubwa kama vile Cristiano Ronaldo wa Ureno, Lionel Messi wa Argentina, mfumaji Diego Costa ambaye ni mzawa wa Brazil na raia wa Uhispania; pamoja na kocha Jose Mourinho ambaye ni mzawa wa Ureno, wamewahi kushtakiwa kwa makosa hayo.

Ancelotti alirejea Uingereza mnamo 2019 baada ya kuwaongoza Chelsea kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2009-10.

Kocha huyo mzawa wa Italia aliongoza Everton kuwalazimishia Liverpool sare tasa katika gozi la Merseyside lililowakutanisha uwanjani Goodison Park mnamo Juni 21. 2020.

Mbali na Chelsea, Real na Everton, Ancelotti anajivunia pia kudhibiti mikoba ya AC Milan, Chelsea, Paris Saint-Germain (PSG) na Bayern Munich.