• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Anthony Kimani kushikilia tena mikoba ya AFC Leopards baada ya kocha Trucha kujiengua

Anthony Kimani kushikilia tena mikoba ya AFC Leopards baada ya kocha Trucha kujiengua

Na CHRIS ADUNGO

AFC Leopards wamemteua tena mwanasoka wa zamani wa Harambee Stars, Anthony Kimani, kuwa kocha wao baada ya kujiuzulu kwa Tomas Trucha ambaye ni raia wa Jamhuri ya Czech.

Trucha aliagana rasmi na Leopards mnamo Disemba 3, 2020 mwezi mmoja pekee baada ya kupokezwa mikoba ya mabingwa hao mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya.

Kiini cha kuondoka kwa ni hofu ya usalama baada ya kudai kwamba meneja wake raia wa Nigeria, Prince Chaniss alitishiwa maisha na baadhi ya watu wanaojulikana na usimamizi wa kikosi cha Leopards.

Kwa upande wao, Leopards walisikitishwa na tukio hilo na kusema: “Hatua ya kubanduka kulichangiwa na hofu ya kutokuwepo kwa usalama baada ya meneja wake kutishiwa maisha na watu wanaojidai kuwa mashabiki wa Leopards. Hili ni suala lisilokubalika kabisa.”

“Mashabiki wa Leopards ni watu wanaojiheshimu na kuongozwa na nidhamu ya hali ya juu. Kwa sasa, maafisa wa benchi ya kiufundi waliosalia watasimamia kikosi huku tukianza mchakato wa kujaza pengo la Trucha. Tunamshukuru Trucha kwa mchango wake katika kikosi cha Leopards na tunamtakia kila la heri katika taaluma yake kwingineko,” ikaongeza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa Leopards, Dan Shikanda, Kimani atapokezwa sasa mikoba ya kikosi kwa mara nyingine japo kwa muda. Kimani aliwahi pia kushikilia mikoba ya Leopards kuanzia Disemba 2019 baada ya mkufunzi Andre-Casa Mbungo ambaye ni raia wa Rwanda kuondoka kwa madai ya kutolipwa malimbikizi ya mshahara.

  • Tags

You can share this post!

Maraga afungua mahakama ya kisasa Nakuru

Wanaraga wa Kenya Simbas wapata mwaliko wa kucheza dhidi ya...