• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Ari ya Manchester United kucheza Europa yatumbukia nyongo

Ari ya Manchester United kucheza Europa yatumbukia nyongo

Na MWANGI MUIRURI 

HUENDA Manchester United ikose kumaliza ndani ya saba-bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kukabwa sare ya 1-1 na timu ya Burnley.

Sare hiyo iliwakumba katika mechi ambayo ilichezewa katika uga wa Man U wa Old Trafford mnamo Aprili 27, 2024.

Kipenga cha mwisho kutoka kinywa cha refa John Brooks kiliishia katika hali ya machungu kwa mashabiki wa Man U waliposhuhudia uhalisia wa sare hiyo.

Man U ilikuwa imejipa matumaini ya kuibuka washindi baada ya mchezaji Antony Matheus dos Santos kutikisa nyavu kunako dakika ya 79 kabla ya kitumbua kuingizwa mchanga na Zeki Amdouni kupitia mkwaju wa penati katika dakika ya 87.

Shida ilitokea wakati nyani wa Man U, Andre Onana alipomshukishia Amdouni ngumi ya kichwa katika mshikemshike langoni na licha ya refa wa wakati Brooks kuikosa penatli hiyo ya ngumi, refa wa mitandaoni (VAR) Peter Bankes aliihalalisha na ikatolewa.

Matokeo hayo yaliiacha Burnley ikiwa katika eneo la hatari la kushushwa daraja.

Kwa sasa, Burnley iko katika nafasi ya 19 ikiwa na pointi 24 lakini ikiwa na matumaini ya kuponyoka ikiwa itawajibikia mechi tatu iliyosalia nazo huku ikiomba walio juu yake wajikwae.

Hesabu hatari ilibaki kwa Man U ambayo matumaini yake makuu ni kucheza katika dimba la Europa ambalo hushirikisha timu zilizomaliza katika nafasi za tano, sita na saba.

Licha ya kubakia katika nafasi ya sita kwa pointi 54, nyuma yake kuna timu za Newcastle na Chelsea ambazo zinaweza zikaipiku kwa wakati wowote.

Matokeo hayo ya sare na Burnley yamezua wasiwasi kwamba huenda Man U ijipate ikishuka hadi nafasi ya tisa, hali ambayo itawasononesha mashabiki wake si haba.

Hata hivyo, Man U kinyume na timu hizo nyingine iko na mwanya wa kushiriki dimba hilo la Europa kupitia kushinda taji la FA ambapo iko katika awamu ya nusu fainali.

Lakini kiwewe ni kwamba itavaana na timu ya Man City ambayo kwa sasa iko katika nafasi ya pili kwa pointi 76 katika jedwali linaloongozwa na timu ya Arsenal ila tu Man U iko na mechi moja kibindoni inayoweza kuifanya iipiku Arsenal.

Huku ligi hiyo ikiwa katika awamu ya lala salama, ni wazi kwamba msukumamo ungalipo na ni kipenga cha mwisho katika mechi ya 38 kwa kila timu ambacho kitatoa taswira kamili.

  • Tags

You can share this post!

Polo mjanja apeleka mamanzi kibandani badala ya hotelini

Mtulipe pesa zetu tuondoke, wanajopo wa IEBC wasema

T L