Arsenal kutema mabeki wapenda rafu Luiz na Mustafi
Na CHRIS ADUNGO
BAADA ya masihara ya beki David Luiz kuchangia kichapo cha 3-0 ambacho Arsenal walipokezwa na Manchester City katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), kocha Mikel Arteta amedokeza uwezekano wa kikosi chake kuagana na sogora huyo mzawa wa Brazil mwishoni mwa msimu huu.
Katika mchuano huo, Luiz aliyetokea benchi kujaza pengo la Pablo Mari aliyepata jeraha katika kipindi cha kwanza, alishindwa kudhibiti mpira aliopokonywa na Raheem Sterling kabla ya masihara yake kuchangia penalti iliyofungwa na kiungo Kevin de Bruyne.
Kwa mujibu wa Arteta, itakuwa vigumu kwa usimamizi wa Arsenal kurefusha mkataba wa Luiz ambaye kipindi cha kuhudumu kwake uwanjani Emirates kinatazamiwa kutamatika rasmi mwishoni mwa msimu huu.
Nyota huyo ambaye pia amewahi kuvalia jezi za Paris Saint-Germain (PSG) nchini Ufaransa, aliingia kambini mwa Arsenal mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuagana rasmi na Chelsea.
Beki mwingine ambaye anatarajiwa kuagana na Arsenal mwishoni mwa msimu huu ni Shkodran Mustafi. Hatua hiyo itamsaza Arteta katika ulazima wa kuisuka upya idara yake ya ulinzi na hawa ni miongoni mwa mabeki ambao huenda akashawishika kusajili:
Thiago Silva
Beki huyu mzawa wa Brazil anatarajiwa kuagana na PSG mwishoni mwa msimu huu baada ya kipindi cha miaka minane ambayo imemshuhudia akinyanyulia miamba hao wa soka mataji saba ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).
Licha ya umri wake mkubwa wa 35, Silva ataleta tajriba ambayo Arteta atahitaji zaidi kambini mwa Arsenal ambao watalazimika kuwapiku Tottenham Hotspur na Everton wanaowania pia maarifa ya difenda huyo.
Dayot Upamecano
Licha ya kuwa na umri wa miaka 21 pekee, beki huyo wa RB Leipzig ya Ujerumani amekuwa kivutio cha Arsenal kwa kipindi kirefu na Barcelona.
Leipzig wamefichua bei ya sogora huyu kuwa Sh6.3 bilioni, fedha ambazo Arsenal walishindwa kutoa msimu jana kwa minajili ya huduma za Upamecano. Sogora huyu aliyesajiliwa na Leipzig miaka mitatu iliyopita sasa angali na mkataba wa miezi 18 pekee kambini mwa kikosi hicho.
Daniele Rugani
Nyota huyu mwenye umri wa miaka 25 alianza kuhusishwa na uwezekano wa kutua Arsenal mwanzoni mwa msimu uliopita. Arsenal walishawishika kumsajili Luiz mwanzoni mwa msimu huu baada ya uhamisho Rugani hadi uwanjani Emirates kugonga mwamba.
Difenda huyu wa Juventus na timu ya taifa ya Italia anawaniwa pia na Leicester City inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Hadi kufikia sasa, Rugani amewajibishwa katika mechi saba pekee kambini mwa Juventus ambao wamekuwa mwepesi wa kumchezesha Matthijs de Ligt na Leonardo Bonucci chini ya kocha Maurizio Sarri.
Jerome Boateng
Arsenal wamefichua kiu ya kumsajili Boateng ambaye amewaomba Bayern Munich nchini Ujerumani kumwachilia asake hifadhi mpya mwishoni mwa msimu huu baada ya kukosa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha miamba hao wanaonolewa na kocha Hansi Flick.
Bayern tayari wamefichua kwamba hawatakuwa radhi kurefusha mkataba wa Baoteng ambaye kwa sasa hupokezwa mshahara wa Sh28 milioni kwa wiki. Hadi kufikia sasa, Boateng amewajibishwa na Bayern katika jumla ya mechi 31 za mapambano yote ya msimu huu.
Samuel Umtiti
Kwa pamoja na Man-United na Tottenham, Arsenal wamo katika vita vya kuwania huduma za beki huyu wa Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa.
Umtiti, 26, amewachezea Barcelona katika jumla ya mechi 17 zilizopita na wepesi wake wa kupata majeraha mabaya ya mara kwa mara huenda ukawachochea Barcelona kumwachilia mwishoni mwa msimu huu.
Kalidou Koulibaly
Nyota huyu mzawa wa Senegal angali na mkataba wa miaka mitatu na Napoli ambao wamefichua kwamba watakuwa radhi kumuuza kwa kima cha Sh14 bilioni.
Koulibaly ambaye pia anawaniwa na Tottenham na Man-United aliingia katika orodha ya mabeki wanaoviziwa na Arsenal mwanzoni mwa msimu huu baada ya kuridhisha zaidi katika mechi mbili za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) zilizowakutanisha na Liverpool.