Michezo

Arsenal kuvunja benki kumsajili Zaha

June 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

KOCHA Unai Emery wa Arsenal amewataka wasimamizi wa kikosi hicho kuvunja benki na kujinasia huduma za mshambuliaji matata wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ivory Coast, Wilfried Zaha, 26.

Emery alishuhudia bajeti yake kwa minajili ya kusajili wachezaji wapya muhula huu ikipunguzwa hadi Sh6.5 bilioni pekee baada ya Arsenal kushindwa kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Baada ya kuambulia nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Arsenal pia walikomolewa na Chelsea kwenye fainali ya Europa League ambapo ushindi ungewashuhudia wakinogesha kampeni za UEFA muhula ujao.

Hata hivyo, Emery ambaye ni mzawa wa Uhispania ameapa kuwasukuma zaidi vinara wa Arsenal kumwongezea hela zitakazomwezesha kujitwalia maarifa ya Zaha ambaye Palace wapo radhi kumwachilia kwa kima cha Sh7.7 bilioni.

Zaha ambaye amewahi kukiri kuwa shabiki sugu wa Arsenal tangu utotoni, amejivunia kampeni za kuridhisha kambini mwa Palace kwa jumla ya misimu mitano iliyopita.

Kulingana na Emery, ujio wa Zaha utamwezesha kulijaza vilivyo pengo la Aaron Ramsey aliyeyoyomea Juventus, Italia mwishoni mwa msimu huu.

Zaha aliyetafuta uraia wa Ivory Coast mnamo 2016 baada ya kukosa nafasi ya kuwajibishwa mara kwa mara katika timu ya taifa ya Uingereza, kwa sasa yuko nchini Misri kwa nia ya kuitambisha nchi yake kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON).

Kikosini

Alikuwa Jumatatu sehemu ya kikosi cha Ivory Coast ambacho kilichuana na Bafana Bafana ya Afrika Kusini katika mchuano wa Kundi D.

Nguli wa Arsenal, Ray Parlour pia amewataka vinara wa kikosi hicho kujinyima zaidi na kumsajili Zaha kwa imani kwamba atawarejesha kileleni mwa EPL msimu ujao.

“Arsenal kwa sasa hawapo katika kiwango sawa na Manchester City au Liverpool ambao walimwaga fedha sokoni na kujinasia huduma za wanasoka mahiri zaidi katika kipindi cha misimu miwili iliyopita,” akatanguliza Parlour.

“Liverpool kwa mfano, walitambua udhaifu wao katika safu ya ulinzi na wakawajitwalia maarifa ya beki Virgil van Dijk na kipa Alisson Becker kwa gharama kubwa. Ajabu ni kwamba hakuna mtu yeyote kwa sasa anayezungumzia gharama ya wachezaii hao wawili kwa sababu matokeo yao yanaonekana klabuni,” akaongeza.

Mbali na Zaha, Arsenal pia wanayahemea maarifa ya beki Kieran Tierney, 22, ambaye anatarajiwa kuagana rasmi na Celtic ya Scotland kwa kima cha Sh3.5 bilioni wiki hii.