• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:27 AM
Arsenal yaendeleza maangamizi ikipanda viwango vya juu

Arsenal yaendeleza maangamizi ikipanda viwango vya juu

Na MWANGI MUIRURI

KLABU ya Arsenal iliponyoka aibu ya kutimuliwa kutoka dimba la Klabu Bingwa Ulaya (Uefa) na timu ya FC Porto baada ya kuibuka mshindi 4-2 kupitia mikwaju ya penalti.

Hali hii iliudhi kwa kiwango kikuu mashabiki wa Manchester United hasa katika mji wa Karatina, Kaunti ya Nyeri ambapo mshirikishi wao, James Ngunjiri, aliteta kwamba kelele za wafuasi wa Arsenal zitasumbua dunia nzima.

“Walipopaa hadi juu ya jedwali mnamo Jumapili baada ya Liverpool na Manchester City kutoka sare, hao mashabiki walizindua misururu ya maringo na makelele wakijiita ‘Ndovu juu ya mti’ na kutudunisha wakisema watatwaa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL),” akasema Bw Ngunjiri.

Aliongeza matarajio yao yalikuwa ni kwamba wazimwe domo na Porto lakini The Gunners wakaponyoka.

“Sasa sisi tunasinyika si haba na nawasihi watupe amani,” akasema shabiki huyo wa Manchester United.

Licha ya hayo, alisema amekubali matokeo kwa msingi wa uanaspoti huku akiitakia timu hiyo ya mkufunzi Mikel Arteta vichapo vikifuatana katika mechi zijazo.

Seneta Maalum Karen Nyamu alisema: “Wanabunduki wakishuka dimbani, watu wa Man U wanafaa kuwa mashimoni kunakowahusu.”

“Tuko juu ya meza na pia ‘Ndovu’ ambaye pia ni sisi, yuko juu ya mti. Wanaotusemasema wako wapi? Wana nini?”

Timu hizo ziliingia uwanjani Emirates ambao ndio nyumbani kwa Arsenal huku Porto ambayo kwa jina la majazi inaitwa Dragon, ikiwa guu moja mbele kwa ushindi wa 1-0 waliopata katika mkondo wa kwanza.

Mkondo wa marudiano mnamo Jumanne ulikuja Arsenal ikiwa chini ya shinikizo za ulazima wa kushinda kwa ubora wa magoli mawili ili kusonga katika mkwaruzano wa robo-fainali.

Lakini hilo halikuwezekana kwa kuwa Arsenal katika muda wa kawaida ilipata goli moja kunako dakika ya 41 kupitia mchezaji Leandro Trossard.

Bao hilo halikutosha kwa kuwa ujumla uliishia kuwa sare ya 1-1 hivyo basi kusukuma mtanange huo hadi muda wa ziada na ambapo mkabano uliishia nguvu sawa.

Ndipo ikawa mshindi asakwe kupitia mikwanju ya penalti na ambapo Arsenali iliibuka na ushindi wa mabao 4-2.

Vijana hao wa Porto chini ya kocha Sergio Paulo Marceneiro da Conceicao waliwahemesha Arsenal na pia wakakinga michuma yao kwa ustadi mkuu huku mara kwa mara wakiishia Arsenal aibu ya kulimwa wakiwa katika uwanja wa nyumbani.

Timu hiyo ya FC Porto ambayo katika ligi ya Ureno iko nambari ya tatu ikiwa na pointi 46, hii ikiwa ni nyuma ya Sporting (69) na Benfica (61), katika Ligi kuu ya Uingereza Arsenal nayo ndiyo kidedea ikiwa na pointi 64, ikiitwa ndovu juu ya mti.

Katika awamu ya kwanza ilipigwa goli hilo la kipekee katika dakika ya 90+4 kutoka guu la Wanderson Rodrigues do Nascimento Galeno wa miaka 26, raia wa Brazil.

Lakini katika mtanange huu wa marudiano alijipata amezamisha timu yake baada ya kushikiwa penalti yake na nyani wa Arsenal, David Raya.

Mkufunzi wa Arsenali Mikel Arteta tayari alikuwa amekiri kwamba mtanange huo ulikuwa uwe mtihani mkuu kwa vijana wake lakini akiahidi kwamba “mtashuhudia nguvu ugani Emirates ambazo  kuziona maishani mwenu, kelele zitakuwa za kichaa na mazingara yatakuwa ya mauaji”.

Hali iliishia kuwa hivyo mashabiki wa Arsenal wakionekana kushangilia kwa makali na hisia thabiti za upendo.

Katika awamu ya kwanza Arsenali licha ya kutawala umiliki wa mpira kwa asilimia 65 dhidi ya 35 ya Porto, haikuwa na hata shuti moja lililolenga michuma.

Katika mechi ya usiku wa kuamkia leo Jumatano Arsenal pia ilithibiti umiliki kwa asilimia 59 dhidi ya 41 huku Porto ikipiga mashuti 10 ya kujaribu magoli dhidi ya 14 ya wapinzani. Arsenal ilitandaza pasi 572 dhidi ya 418 za Porto.

Penalti za Arsenal zilifungwa na nahodha Martin Odegard, Kai Havertz, Declan Rice, na Bukayo Saka.

  • Tags

You can share this post!

Waapa kuacha pombe baada ya kupofuka ulevini

Monda roho mkononi Seneti ikianza kumjadili

T L