Michezo

Arsenal, Man City wala kavu katika kipute cha Klabu Bingwa Ulaya

April 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA LABAAN SHABAAN

BAYERN Munich ilishinda kwa bao moja nunge dhidi ya Arsenal ugani Alianz Arena ili kuwabandua Waingereza nje ya Mashindano ya Klabu Bingwa Ulaya katika hatua ya robo fainali.

Na huko ugani Etihad, miamba Manchester City walibanduliwa na Real Madrid kupitia mikwaju ya penalti baada ya mambo kuishia sare ya jumla ya mabao 4-4 kwenye muda wa kawaida na wa ziada.

Bao la Joshua Kimmich lilishikilia miamba wa Ujerumani kufikia dakika ya 94 hadi refa akapuliza kipenga kuwarejesha Wanabunduki nyumbani Uingereza wakiwa hoi bin taabani.

Bayern Munich wamesonga mbele kuingia nusu fainali baada ya kuibuka kidedea kwa jumla ya mabao 3 – 2.

Juma lililopita, timu hizi ziliambulia sare ya mabao mawili na kupisha mechi ya marudiano usiku wa Jumatano nchini Ujerumani.

Beki wa kulia Kimmich alipiga shuti kali la kichwa kuunganisha krosi ya Raphael Guirrero dakika ya 63 na kuyumbisha wavu.

Arsenal ilitawala mchezo katika kipindi cha kwanza na sehemu kubwa ya kipindi cha pili ila walishindwa kucheka na wavu.

Ubutu wa Arsenal uliwapa vijana wa Thomas Tuchel matumaini ya kurudi kwenye mchezo kipindi cha pili.

Matokeo ya mchuano huu yameongeza chumvi kwenye kidonda cha Arsenal siku chache baada ya kulimwa 2 – 0 na Aston Villa katika Ligi Kuu ya Kandanda Uingereza (EPL)

Sasa, matumaini ya Arsenal kutwaa kombe la EPL baada ya miaka 20 yananing’inia kwenye uzi mwembamba licha ya kufana sana msimu huu.

Hii ni baada ya bingwa mtetezi Manchester City kurudi kileleni mwa jedwali zikisalia mechi chache msimu kukamilika.