Michezo

Arsenal yaonyesha ukatili kwa kusukumia wapinzani magoli 25 tangu mwaka uanze

February 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

ARSENAL waliweka wazi azma yao ya kutawazwa wafalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu baada ya kukomoa Newcastle United 4-1 mnamo Jumamosi usiku ugani Emirates.

Ushindi huo ulikuwa wa sita mfululizo kwa masogora hao wa kocha Mikel Arteta kusajili ligini.

Sasa wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 58, moja nyuma ya mabingwa watetezi Manchester City na mbili zaidi nyuma Liverpool wanaoselelea kileleni baada ya kutandaza pia michuano 26.

Mabao ya Arsenal yalijazwa kimiani kupitia kwa Jakub Kiwior, Bukayo Saka, Kai Havertz na Sven Botman aliyejifunga.

Newcastle ambao wanakamata nafasi ya nane kwa alama 37, walifutiwa machozi na fowadi wa zamani wa Arsenal, Joe Willock.

Kufikia wakati kama huu msimu uliopita, matumaini ya Arsenal kunyanyua taji la EPL yalikuwa yameanza kudidimia baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi Brentford na kukubali vichapo vya 1-0 na 3-1 kutoka kwa Everton na Man-City mtawalia.

Hatimaye walikamilisha kampeni za muhula huo katika nafasi ya pili kwa alama 84, tano nyuma ya Man-City licha ya kufungua pengo la pointi nane kileleni mwa jedwali kuelekea mwisho wa Januari 2023.

Japo Arsenal walianza msimu huu kwa kusuasua, vijana hao wa Arteta wanazidi kuimarika huku wakijizolea jumla ya mabao 25 na kuruhusu wapinzani kutikisa nyavu zao mara tatu pekee kutokana na mechi sita zilizopita za EPL.

Zaidi ya kucheza soka safi ya kuvutia sawa na waliyoionyesha mwanzoni mwa msimu jana, miamba hao wanajituma na kutawaliwa na kiu ya kushinda kila mchuano. Mara ya mwisho kwa sifa hiyo kujidhihirisha kambini mwa Arsenal ni 2003-04 walipotia kapuni taji la EPL.

Ufufuo wa makali yao umeonekana zaidi kupitia jinsi wanavyowania mipira ya hewani na kutegemea mabeki wao – Gabriel Magalhaes, Ben White, Kiwior na William Saliba – kufunga mabao kupitia kona na mipira ya ikabu. Hakuna timu nyingine ambayo imepachika wavuni mabao mengi zaidi kutokana na mipira ya sampuli hiyo msimu huu kuliko Arsenal (19).

Walidhibiti mchezo kuanzia mwanzo na kuwafanya Newcastle kutowaelekezea kombora lolote katika kipindi kizima cha kwanza. Mara ya mwisho kwa Newcastle kuweka rekodi hiyo mbovu ni Machi 2014.

Jumatatu itakuwa zamu ya West Ham United kualika Brentford ugani London Stadium wakilenga kukomesha fomu mbaya ambayo imewashuhudia wakipoteza mechi tatu mfululizo zilizopita ligini.

Kufikia sasa, West Ham wanajivunia alama 36 huku pengo la pointi 11 likiwatenganisha na Brentford ambao wamepoteza michuano minne kati ya tano zilizopita katika EPL.

West Ham hawajawahi kushinda pambano lolote kati ya manane yaliyopita tangu wapepete Arsenal 2-0 katika EPL ugani Emirates mwishoni mwa mwaka jana.

Kikosi hicho cha kocha David Moyes kilidenguliwa na Bristol City kwenye Kombe la FA mwezi jana na hakijashinda mechi sita mfululizo ligini huku kikiambulia sare dhidi ya Brighton (0-0), Sheffield United (2-2) na Bournemouth (1-1) kabla ya kupoteza dhidi ya Manchester United (3-0), Arsenal (6-0) na Nottingham Forest (2-0).