Michezo

Arteta amuomba Auba kusalia Arsenal

August 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MKUFUNZI Mikel Arteta amemsihi fowadi na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang kutia saini mkataba mpya utakaomshuhudia akistaafu uwanjani Emirates na kuingia katika historia ya kuwa miongoni mwa wanasoka nguli wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Vinara wa Arsenal wanatazamiwa kumpokeza Aubameyang kandarasi mpya ya miaka mitatu wiki hii katika maagano yatakayomshuhudia akitia kapuni kima cha Sh35 milioni kwa wiki.

Aubameyang aliwazamisha Chelsea kwa mabao 2-1 na kusaidia Arsenal kutwaa ubingwa wa Kombe la FA wikendi iliyopita na hivyo kujikatia tiketi ya kushiriki Europa League msimu ujao. Mfumaji huyo angali na mwaka mmoja pekee katika mkataba wake na Arsenal.

“Kufunga ni kitu kigumu zaidi katika soka. Lakini Aubameyang amefanya ufungaji wa mabao kuonekana kitu rahisi sana, hasa alivyopachika wavuni bao la pili na la ushindi dhidi ya Chelsea. Arsenal ni kikosi ambacho kimekuwa na historia ya kujivunia huduma za wanasoka mahiri, na Aubameyang anastahiki kuanza kulinganishwa na majina hayo kwa sasa,” akasema Arteta.

Wachezaji waliokuwa wakirejelewa na Arteta ni Thierry Henry, Dennis Bergkamp na Ian Wright.

“Kwa kushinda mataji, ataanza kuwakaribia wanasoka hao na tuna matumaini ya kujivunia huduma zake kwa muda mrefu.”

Arsenal wana kifungu kinachowaruhusu kuongeza mkataba wa Aubameyang kwa kwa msimu mmoja zaidi wa 2021-22 kuanzia Disemba 31.

Fungu zima linalowapa pia ruhusa ya kumlipa Aubameyang kitita cha Sh2.8 bilioni mara moja kwa msimu mzima badala ya kumpokeza mshahara wa Sh56 milioni kwa wiki.

Arteta aliteuliwa kuwa kocha wa Arsenal mnamo Disemba 2019 na akaanza kumhimiza Aubameyang ambaye ni mzawa wa Gabon kujitahidi zaidi hata akiwa nje ya uwanja.

“Tatizo kubwa zaidi lilikuwa kumshawishi Aubameyang kufanya kazi kwa namna tulivyotaka aitende. Tuliamini kwamba hilo lingemvunia tija zaidi na heshima, awe kivutio cha mashabiki, watu waliopo karibu naye na wachezaji wenzake,” akasema Arteta.

Katika mahojiano yake na gazeti la The Sun mnamo Mei 10, 2020, Aubameyang alisema anatawaliwa na kiu ya kutimiza ahadi ya kuchezea Real Madrid kwa kuwa ndiyo maneno ya mwisho aliyomwambia babu yake kabla ya kuaga dunia.

Awali 2016 akichezea Borussia Dortmund, aliungama kuwa aliwahi kuapia babu yake kwamba atachezea Real siku moja kabla ya kustaafu kwenye ulingo wa soka.

Aubameyang pia alikiri kwamba mtindo wake wa kusherehekea mabao kwa kupiga vichwangomba (somersaults) ni katika juhudi za kuiga aliyekuwa nguli wa soka uwanjani Santiago Bernabeu, Hugo Sanchez.

Sanchez ambaye ni mzawa wa Mexico, aliwahi kufungia Real jumla ya mabao 208 kutokana na mechi 283 na kusaidia kikosi hicho kutwaa mataji matano ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kati ya 1985 na 1992.

Mnamo Juni 15, 2020 Aubameyang alisema kuwa maamuzi ya ama kutia saini mkataba mpya kambini mwa Arsenal au kuagana na kikosi hicho ndiyo “magumu na muhimu zaidi” katika taaluma yake ya usogora.

“Bado sijapokea ofa yoyote rasmi ambayo imeanza kunishawishi kutaka kubanduka Arsenal. Hata hivyo, zipo tetesi za kila aina zinazonihusisha na klabu mbalimbali za bara Ulaya ikiwemo Inter Milan, Real Madrid na Barcelona,” akatanguliza Aubameyang.

“Niliwahi kuzungumza na Arsenal miezi michache iliyopita kuhusiana na tetesi hizo, na wanafahamu sababu ambazo hakuna chochote kimefanyika hadi kufikia sasa,” akasema.

“Ni kipindi muhimu zaidi katika taaluma yangu na ningependa kuwa mkweli kwa kila mmoja wa mashabiki wangu,” akaendelea.

“Arsenal ndio wenye ufunguo wa mustakabali wangu kisoka. Ni juu yao kufanya kazi yao, na baada ya hapo tutaona namna mambo yatakavyokwenda. Bila shaka maamuzi ya kusalia au kuondoka Emirates ni magumu sana kwangu kufanya peke yangu,” akaongeza.