Michezo

Asamoah Gyan astaafu soka ya kimataifa

May 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA CECIL ODONGO

NYOTA wa timu ya taifa la Ghana Asamoah Gyan ametangaza kustaafu soka ya kimataifa baada ya kuchezea timu ya taifa ya Ghana kwa miaka 16.

Gyan ambaye ni mfungaji bora wa The Black Stars, kupitia taarifa alisema hataki kushirikishwa kwenye fainali ya Taifa Bingwa Barani Afrika (AFCON) itakayong’oa nanga Juni 21 mjini Cairo, Misri hasa baada ya habari kuchipuka kwamba amepokonywa unahodha.

“Baada ya kushauriana na familia yangu na timu ya taifa na kama mwanakabumbu na nahodha wa Black Stars nimeamua kustaafu soka. Siwezi kudanganya kwamba nitafurahikia uamuzi wa kocha kumpa mchezaji mwengine utepe wa unahodha iwapo nitakuwa timuni

“Naomba kujiondoa katika timu ya taifa milele na sidhani kutokwepo kwangu kutaonekana kama usaliti kwa taifa langu. Nitaendelea kutumikia Ghana kama mfanyabiashara anayewekeza katika miradi mbalimbali,” ikasema taarifa ya mshambulizi huyo mweledi ambaye aliskata soka katika baadhi ya ligi za maarufu duniani

Gyan amekuwa mchezaji tegemeo kwa Black Stars hasa baada ya kucheza mechi yake ya kwanza ya kimataifa mwaka wa 2003 akiwa na umri wa miaka 17 pekee, wakati ambao pia alifunga bao lake la kwanza kwa timu ya taifa, Ghana ikicheza dhidi ya Somalia.

Hata hivyo, kumbukumbu itakayoacha taathira ya milele kwenye akili za jabali huyo wa soka ni kupoteza mkwaju wa penalti dakika ya mwisho ya mechi wakati Ghana ikimenyana na Uruguay katika robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka wa 2010 nchini Afrika Kusini.

Ghana iliishia kupoteza mechi hiyo baada ya muda wa ziada kukamilika bila magoli na mshindi akaamuliwa kupitia mikwaju ya penalti.

Kando na hayo, Gyan pia alishiriki makala ya Kombe la Dunia miaka ya 2006, 2010 na 2014.