Michezo

Askofu Yohana aitakia Arsenal ushindi dhidi ya Brentford

March 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MWANGI MUIRURI Na MASHIRIKA

ASKOFU Danson Gichuhi almaarufu Yohana ambaye amegonga vichwa vya vyombo vya habari kwa kukemea mapepo kutoka kwa waumini wake wa kike kwa njia tata, anaitakia klabu yake ushindi.

Yohana ni shabiki sugu wa klabu ya Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

“Ninaitakia klabu ya Arsenal itakapovaana na Brentford,” akasema alipohojiwa na Taifa Spoti mnamo Ijumaa akiwa mjini Murang’a.

Kanisa la Yohana linafahamika kama Christian Committed Gospel Church na lina matawi Nakuru, Murang’a, na Kirinyaga.

Arsenal itacheza dhidi ya Brentford ugani Emirates mnamo Jumamosi kuanzia saa mbili na nusu usiku saa za Afrika Mashariki.

Klabu hiyo inapigiwa upatu kuendelea kugawa dozi kali kwa wapinzani.

Vijana wa kocha Mikel Arteta watashuka dimbani dhidi ya Brentford kwa mechi ya raundi ya 28 ya EPL msimu huu.

Ni wikendi ambayo pia itashuhudia mechi kadhaa moto ikiwemo viongozi Liverpool kupimwa makali yao na nambari mbili Manchester City, Manchester United (sita) kualika Everton (16), Aston Villa (nne) kutoana jasho na Tottenham (tano) nao Chelsea (11) watavaana na Newcastle (nane).

Wanabunduki wa Arsenal wataingia mechi dhidi ya Brentford na motisha tele baada ya kubomoa Crystal Palace 5-0, Nottingham Forest 2-1, Liverpool 3-1, West Ham 6-0, Burnley 5-0, Newcastle 4-1 na Sheffield United 6-0 katika saba mfululizo ligini.

Watakutana na Bees ambao hawana ushindi dhidi ya Arsenal mara tano mfululizo kwenye mashindano yote na pia wameokota alama moja kutoka nne zilizopita msimu huu.

Ikiwa Arsenal watavuna alama zote inavyotarajiwa, basi vijana hao wa kocha Mikel Arteta wataruka hadi kileleni mwa jedwali wakisubiri matokeo ya Jumapili kati ya Liverpool na City.

Liverpool wanaongoza kwa alama 63 na kufuatiwa na City (62) na Arsenal (61).

Arsenal na Brentford watakaokuwa wakikabiliana kwa mara ya 20 katika historia yao, watategemea mawinga Bukayo Saka na Yoane Wissa katika utafutaji wa mabao.

Hata hivyo, Arteta huenda akatumia Gabriel Jesus ama Leandro Trossard kwa sababu Saka pamoja na Gabrieli Martinelli, Oleksandr Zinchenko, Takehiro Tomiyasu walikuwa na ishu kutokana na ugonjwa ama jeraha.

Mchezaji wa Arsenal Leandro Trossard aingia uwanjani kujaza nafasi ya Declan Rice wakicheza dhidi ya wenyeji Sheffield United ugani Bramall Lane mnamo Machi 4, 2024. PICHA | REUTERS

Kipa David Raya atakuwa shabiki kwa sababu yuko Arsenal kwa mkopo kutoka kwa Brentford kwa hivyo Aaron Ramsdale anatarajiwa kuwa michumani. Kocha Thomas Frank pia ana orodha ndefu ya wachezaji atakaokosa wakiwemo majeruhi Bryan Mbeumo, Kevin Schade, Aaron Hickey, Ethan Pinnock, Rico Henry na Josh Dasilva, ingawa mvamizi matata Ivan Toney yupo kuhangaisha Arsenal wanaommezea mate.

United watakuwa mawindoni kudumisha rekodi nzuri dhidi ya Everton itakayozuru uga wa Old Trafford katika mchuano wa kufungua siku Jumamosi.

Vijana wa kocha Erik ten Hag wamelemea Everton mara nne mfululizo katika mashindano yote.

Walipoteza mbili zilizopita ligini dhidi ya Fulham na City kwa hivyo wanatafuta kujinyanyua. Everton haina ushindi mara saba mfululizo msimu huu.

Mechi kati ya Villa na Tottenham na pia Chelsea na Newcastle zinaweza kuenda upande wowote.

Ratiba:

Jumamosi – Manchester United vs Everton (3.30pm), Crystal Palace vs Luton Town (6.00pm), Bournemouth vs Sheffield United (6.00pm), Wolves vs Fulham (6.00pm), na Arsenal vs Brentford (8.30pm).

Jumapili– Aston Villa vs Tottenham (4.00pm), West Ham vs Burnley (5.00pm), Brighton vs Nottingham Forest (5.00pm), Liverpool vs Manchester City (6.45pm); Machi 11 – Chelsea vs Newcastle (11.00pm).