• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 5:36 PM
Askofu Yohana amtaja Kai Havertz kuwa ni mwokozi pale Arsenal

Askofu Yohana amtaja Kai Havertz kuwa ni mwokozi pale Arsenal

Na MWANGI MUIRURI

WAKATI mchezaji Kai Havertz alinunuliwa kutoka Chelsea mwaka 2023 kuwajibikia timu ya Arsenal katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kima cha Dola Milioni 65, mashabiki wengi wa timu hiyo yake mpya hawakuridhika.

Kwa mitandao, walikesha kumdhalilisha wakimkejeli jinsi alivyokuwa mzembe, mbutu na wa kuhujumu ari ya Arsenal kutwaa ligi.

Kocha Mikel Arteta hakuwasikiliza mashabiki na kwa kila mechi, jina lake lilikuwa linawekwa miongoni mwa 11 wa kuanza, mashabiki wakibakia kulia na kukashifu.

Lakini mui huwa mwema. Mashabiki wao hao waliojaliwa kila aina ya kelele mitandaoni ndio hao kwa sasa ambao hawashikiki wakimsifu Havertz kuhusu jinsi ambavyo amekuwa mwangamizi na tegemeo katika safari ya kutwaa taji la EPL ambalo limewakwepa kwa miaka 20 sasa.

Kwa hesabu rahisi, Arsenal ilishinda taji hilo la EPL Havertz akiwa mtoto wa umri wa miaka minne na amekua, akaiva hadi akafikia uwezo wa kuja kuisaidia kulitwaa tena, mara hii akiwa mchezaji.

Alizaliwa Juni 11,1999, katika mtaa wa Aachen nchini Ujerumani na ari yake ya kuwa mchezaji kabumbu ilitambuliwa utotoni mwake na babu yake na aliyemunoa hadi akakomaa ambapo hadi sasa kwa msimu huu, ametingizi Arsenal nyavu mara 12.

“Huyu ni mwanasoka anayependa kucheza piano na ambaye kumuelewa ni vigumu. Amenifanya nimheshimu kocha Arteta kwa kiwango kikuu kwa kuona usogora fiche wa Havertz ambao sisi kama mashabiki hatukuwa tunauona. Lakini weledi wake unazidi kujiangazia tukishuhudia na kutufanya tufyate midomo ya kumsuta,” asema Askofu Yohana Gichuhi wa kanisa la Christian Committed Gospel Church nchini Kenya.

Askofu Yohana anasema mabao ya Havertz ya usiku wa Aprili 23, 2024, dhidi ya Chelsea “yalinifanya kutambua kwamba huyu mchezaji ako na nyota iliyo baraka ya moja kwa moja kutoka kwa Mungu na huu upole wake ndio sisi hudhania ni uzembe ilihali ni mwokozi asiyependa kubishana”.

Askofu Danson Gichuhi almaarufu Yohana. PICHA | MWANGI MUIRURI

Askofu Yohana anasema kwamba wachambuzi katika vyombo vya habari nchini Ujerumani walimpa Havertz jina la majazi la Alleskonner, maana yake ikiwa ni mtu ambaye anaweza akafanya chochote (akiwa na mpira guuni).

Askofu anasema kwamba chochote hujumlisha pamoja hata kupoteza nafasi ya wazi, kufunga goli katika hali yoyote kwa vyovyote vile na pia hata kusaidia wenzake wafunge magoli “na hayo yote tumeyashuhudia akiyafanya mbele ya macho yetu”.

Akiwa na umri wa miaka minne pekee, Havertz alijiunga na Klabu ya Alemannia Mariadorf karibu na kwao nyumbani kabla ya kujiunga na taasisi ya ukuzaji vipaji ya Bayer Leverkusen akiwa wa miaka 11.

Babu yake Havertz akijulikana kama Mzee Richard, ndiye alikuwa mwenyekiti wa timu hiyo ya Alemannia Mariadorf na ndiye humininiwa sifa kama aliyemfanya mchezaji huyo kujielewa na kuwa na malengo ya kuafikia makuu ugani.

Aliingia katika kumbukumbu za Leverkusen mwaka wa 2016 kama mchezaji mchanga zaidi kuchezea timu hiyo katika ligi ya Ujerumani ya Bundesliga akiwa na miaka 17.

Seneta maalum Bi Karen Nyamu anasema kwamba wasiopenda kufanya utafiti ndio hawawezi wakamuelewa Havertz.

“Kuna mashabiki ambao kueleewa mpira kwao ni kusikia tu timu yao imefunga mabao ya kubebwa kwa gunia. Mashabiki ambao wakiingia ugani kushabikia, wanangojea tu waanze kuwaumiza wapinzani. Hawaelewi kwamba mchezo wa soka huwa na matokeo aina nne—ushinde, ushindwe, iwe sare au mechi itupiliwe mbali,” asema Bi Nyamu.

Anasema kwamba mashabiki wakomavu wangekuwa wamejua kwamba Havertz katika msimu wa 2018-19 akiwajibikia klabu inayoshiriki Bundesliga, alitikisa nyavu za wapinzani mara 17 kwa niaba ya Leverkusen na akatajwa kuwa mchezaji bora zaidi wa ligi hiyo mwezi wa Aprili 2019.

Bi Nyamu anasema kwamba wachambuzi wangekuwa wameng’amua ukweli wa mambo kwamba Havertz hupenda sana punda na ambapo huwa na mbuga yake ya wanyama hao.

“Hii ina maana kwamba Havertz hupata ushawishi wake kutoka kwa bidii ya punda. Na tumemwona katika uwanja akitekeleza sifa za punda katika bidii na ustadi wa kubeba mizigo kwa kuwa sio mara moja huyu aliyechukiwa ametubeba kama Arsenal hadi kwa ushindi,” akasema.

Mchezaji wa Arsenal Kai Havertz asherehekea kufunga bao dhidi ya Chelsea ugani Emirates mnamo Aprili 23, 2024. PICHA | REUTERS

Septemba 2020, Chelsea iliona makali yake na ikamsajili kwa kima cha Dola 72 milioni ambapo yeye ndiye alitinga goli la ushindi katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Manchester City.

Katika mahojiano mbalimbali mitandaoni, Havertz amekiri mara si haba kwamba akilea kipaji chake cha soka, kishawishi chake kikuu kilikuwa timu ya Barcelona ya nchini Uhispania.

Amewataja wanasoka Samuel Eto’o na Ronaldinho kama wachezaji ambao walikuwa wakimpagawisha akiwatazama ugani na akawa na ari ya siku moja kuwa kama wao.

Miongoni mwa wasifu wake ni kwamba ndiye alikuwa wa kwanza kutikisa nyavu mara nyingi katika soka ya wazima Bundesliga akiwa yungali kijitoto cha umru wa miaka 17 na pia akawa msaidizi wa kufungwa kwa goli la Lervekusen la 50,000 na mwenzake Karim Bellarabi wakivaana na timu ya Augsburg katika ligi hiyo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Uchunguzi: Wi-Fi ya bure haifanyi kazi katika kaunti nyingi...

Zaidi ya maskwota 1,200 eneo la Kisauni kufurushwa

T L