Michezo

Aston Villa na Burnley ni nguvu sawa EPL

December 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

ASTON Villa walishindwa kujizolea alama tatu muhimu dhidi ya Burnley katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha uwanjani Villa Park mnamo Alhamisi.

Mechi hiyo ilikuwa ya nne mfululizo kwa Villa kutoshinda katika uwanja wao wa nyumbani. Villa walianza mchuano huo kwa matao ya juu huku wakivurumisha jumla ya makombora 15 kwenye lango la wapinzani wao katika kipindi cha kwanza pekee na kushuhudia mpira ukigonga mwamba wa goli la wageni wao mara mbili.

Beki Matthew Lowton wa Villa alijitahidi na kumnyima Ahmed El Mohamady fursa kadhaa za kufunga huku kipa Nick Pope naye akijituma vilivyo katikati ya michuma ya Burnley na kupangua makombora mazito aliyoelekezwa na mshambuliaji Anwar El Ghazi.

Licha ya kutoshinda mechi hiyo dhidi ya Burnley, Villa walifaulu kuendeleza rekodi nzuri ya kutofungwa katika mechi sita hadi kufikia sasa kwenye EPL.

“Tulipata nafasi nyingi za wazi ambazo zingetuvunia mabao matatu hivi. Yasikitisha kwamba hatuondoka uwanjani na alama zote muhimu. Hata hivyo, vijana walijituma sana na dalili zote zinaashiria uwepo wa nia ya kikosi kufufua makali,” akasema kocha Dean Smith.

Jack Grealish na Tyrone Mings ni miongoni mwa wanasoka wengine waliojitahidi maradufu kwa upande wa Villa bila ya kufaulu kuona lango la wapinzani.

Matokeo ya mechi hiyo yalisaza Villa katika nafasi ya 11 kwa alama 19, tisa zaidi kuliko Burnley wanaoshikilia nafasi ya 19, 2020.

Tangu wapokezwe kichapo cha 5-0 kutoka kwa Manchester City uwanjani Etihad mnamo Novemba 28, 2020, kikosi cha Burnley kinachonolewa na kocha Sean Dyche kimeambulia sare dhidi ya Everton, kushinda Arsenal uwanjani Emirates na kuwakaba Villa koo ugani Villa Park.

Aston Villa wanajiandaa sasa kuwaendea West Bromwich Albion kwenye debi kali ya Midlands mnamo Disemba 20 siku moja kabla ya Burnley kushuka dimbani kumenyana na Wolves uwanjani Molineux.