• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Atwoli aongoza kampeni za kuzima Ruto Magharibi

Atwoli aongoza kampeni za kuzima Ruto Magharibi

Na OSCAR OBONYO Na BENSON MATHEKA

KATIBU Mkuu wa muungano wa vyama vya wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli, ameendesha juhudi za kumpatanisha kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Hatua hiyo imetajwa kuwa miongoni mwa juhudi zake za kumzuia Naibu Rais William Ruto, kupenyeza ushawishi wake wa kisiasa eneo la Magharibi mwa Kenya.

Taifa Jumapili ilibaini kuwa hatua ya Bw Atwoli ni sehemu ya njama pana ya kujenga umoja wa jamii ya Mulembe na tayari vigogo wa kisiasa eneo hilo, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula na Eugene Wamalwa, wamekuwa wakikutana kwa siri kuweka mikakati ya kuunda muungano wa jamii ya Waluhya.

Kulingana na Bw Wetangula, waliamua kufanya mikutano yao kisiri ili kuepuka kuvurugwa na wanaotaka kutimiza maslahi ya kibinafsi.

“Ukweli ni kwamba, tumekuwa tukidharauliwa kama jamii katika siasa za kitaifa kwa miaka mingi. Lakini hii ni sehemu ya historia yetu na siku zijazo zitakuwa tofauti kabisa,” alisema Bw Wetang’ula, ambaye ni seneta wa Bungoma.

Mabw Mudavadi, Wetangula na Wamalwa wamezindua kampeni ya kuunganisha jamii za Waluhya, Teso na Sabaot wanaoishi Bungoma, Busia, Kakamega, Vihiga na Trans Nzoia eneo la Rift Valley.

Duru zilifahamisha Taifa Jumapili kwamba wameunda kundi linaloshirikisha wataalamu kufanikisha juhudi zao.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Ford Kenya, Dkt Eseli Simiyu, ambaye inasemekana ni mmoja wa wanachama wa kamati hiyo, waliamua kuweka mambo yao kisiri hadi wafaulu.

“Kuna mikakati madhubuti inayoendelea lakini samahani, wakati huu tumeamua kufanya mambo chini ya maji.Hii ni kwa sababu kila wakati tunapoeleza wanahabari mipango yetu na kuizungumzia katika mikutano ya hadhara, tunawapatia wapinzani wetu silaha ya kutuvuruga na kutugawanya,” alisema Dkt Eseli.

Viongozi hao watatu na Bw Atwoli, wamekuwa wakikutana kuweka msingi wa kuunganisha eneo la Magharibi kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 na ni kufuatia mikutano hiyo ambapo Bw Wetangula alibadilisha nia ya kumuunga Bw Ruto.

Kiongozi wa wachache katika seneti

Duru zinasema kuwa Bw Atwoli alimpatanisha Bw Wetang’ula na Bw Odinga.

Wawili hao waliokuwa katika muungano wa NASA walitofautiana chama cha ODM kilipombandua Wetang’ula kutoka wadhifa wa kiongozi wa wachache katika seneti.

Wadadisi wanasema Mudavadi,Wetangula na Wamalwa wanahisi kwamba Bw Odinga anaweza kuwasaidia kumzuia Dkt Ruto kupenya katika ngome yao ya kisiasa.

Huku Atwoli akijitwika jukumu la kumzuia Dkt Ruto kutandaza ushawishi wake eneo la Magharibi, Mudavadi, Wetangula na Wamalwa wamekuwa wakihubiri umoja wa jamii ya Mulembe.

Watatu hao wamekuwa wakisafiri kwa ndege moja na kuhudhuria hafla pamoja eneo la Magharibi.

Wiki jana, wakiwa Busia walikiri kwamba wamezindua kampeni ya kukabiliana na watalii wa kisiasa eneo hilo.

“Nasikia kuna watu wanaozunguka hapa wakidai wameteka eneo lote la Magharibi mwa Kenya. Hao wanatarajia kutumia kutengana kwetu kwa miaka mingi na wale wanaotarajia kutumia umaskini wetu watashangaa,” Bw Wamalwa alisema akiwa Butula, akilenga ziara naibu rais amekuwa akifanya eneo hilo.

  • Tags

You can share this post!

MWANAMKE MWELEDI: Aliwafungulia milango wanawake wengine

Wawika nje, baridi bungeni

adminleo