• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 5:20 PM
Auba asema uamuzi wa kuondoka Arsenal unamkanganya

Auba asema uamuzi wa kuondoka Arsenal unamkanganya

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI na nahodha Pierre-Emerick Aubameyang, 30, amesema maamuzi ya ama kutia saini mkataba mpya kambini mwa Arsenal au kuagana na kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndiyo “magumu na muhimu zaidi” katika taaluma yake ya usogora.

Mkataba wa sasa wa nyota huyo mzawa wa Gabon unatazamiwa kutamatika rasmi ugani Emirates mwishoni mwa Juni 2021.

“Bado sijapokea ofa yoyote rasmi ambayo imeanza kunishawishi kutaka kubanduka Arsenal. Hata hivyo, zipo tetesi za kila aina zinazonihusisha na klabu mbalimbali za bara Ulaya ikiwemo Inter Milan, Real Madrid na Barcelona,” akatanguliza Aubameyang.

“Niliwahi kuzungumza na Arsenal miezi michache iliyopita kuhusiana na tetesi hizo, na wanafahamu sababu ambazo hakuna chochote kimefanyika hadi kufikia sasa,” akasema sogora huyo wa zamani wa Borussia Dortmund katika mahojiano yake na runinga moja nchini Ufaransa.

“Ni kipindi muhimu zaidi katika taaluma yangu na ningependa kuwa mkweli kwa kila mmoja wa mashabiki wangu,” akaendelea.

“Arsenal ndio wenye ufunguo wa mustakabali wangu kisoka. Ni juu yao kufanya kazi yao, na baada ya hapo tutaona namna mambo yatakavyokwenda. Bila shaka maamuzi ya kusalia au kuondoka Emirates ni magumu sana kwangu kufanya peke yangu,” akasema

Kufikia sasa, Aubameyang anajivunia kufungia Arsenal jumla ya mabao 61 kutokana na mechi 97 zilizopita tangu abanduke kambini mwa Dortmund mnamo 2018.

Mnamo Machi 2020 kabla ya kipute cha EPL kusimamishwa kwa muda kutokna na janga la corona, kocha Mikel Arteta wa Arsenal alisisitiza kwamba wako tayari “kufanya lolote lililo ndani ya uwezo wao” kuhakikisha kwamba Aubameyang anatia saini mkataba mpya ili asalie ugani Emirates kwa kipindi kirefu zaidi.

Barcelona wanapania kumsajili Aubameyang ili awe kizibo cha kigogo Luis Suarez anayetazamiwa kustaafu mwishoni mwa msimu ujao. Hata hivyo, wataazimia zaidi kumtwaa iwapo watamkosa Lautaro Martinez wa Inter Milan.

Arsenal ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tisa kwa alama kwenye msimamo wa jedwali la EPL wanatarajiwa kuvaana na nambari mbili Manchester City soka ya Uingereza itakaporejelewa mnamo Juni 17, 2020.

  • Tags

You can share this post!

Beyern kutawazwa mabingwa wakiilima Bremen

Sababu za mbunge wa Mvita kupinga agizo la usafirishaji...

adminleo