• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Ayimba sasa ni mkurugenzi wa kiufundi RLF

Ayimba sasa ni mkurugenzi wa kiufundi RLF

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa zamani wa timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa, Benjamin Ayimba ameteuliwa mkurugenzi wa kiufundi wa Shirikisho la Kenya Rugby League (RLF).

Ayimba ambaye ni nahodha wa zamani wa Shujaa atakuwa na jukumu la kuchangia masuala ya kiufundi katika maendeleo ya raga kwenye viwango vya mashinani, klabu za jamii na kitaifa.

Atakuwa pia na wajibu wa kubuni mipango ya kufanikisha matokeo bora ya wachezaji, makocha, marefa na maafisa wa raga ya humu nchini katika viwango mbalimbali.

Ayimba alisimamia kipute cha kwanza cha Rugby League kilichowahi kuandaliwa humu nchini na kutawaliwa na Wolves mnamo Februari 2020 ugani Railway Club, Nairobi.

Mwenyekiti wa RLF, Nyakwaka ‘Quicks’ Adhere amesema kwamba ujio wa Ayimba ni afueni kubwa kwa raga ya humu nchini hasa ikizingatiwa ukubwa wa mafanikio yake katika ulingo wa mchezo huo.

“Anajivunia rekodi ya kipekee katika ulingo wa raga. Tajriba yake uwanjani na uzoefu katika masuala ya uongozi utachangia pakubwa makuzi ya mchezo huu ambao unazidi kukua kwa kasi humu nchini,” akaongeza Nyakwaka.

Kenya wanatazamia kuchuana na Afrika Kusini baadaye mwaka huu katika mchuano wa Rugby League chini ya ukufunzi wa nguli wa raga ya humu nchini, Edward Rombo aliyepokezwa mikoba ya timu ya taifa mnamo Mei 2020.

Chini ya ukocha wa Ayimba, Shujaa walitamalaki duru ya Singapore Sevens katika Raga ya Dunia mnamo Machi 2016.

Akiwa nahodha, aliwahi kuwaongoza Impala Saracens kujitwalia mataji matatu ya Kenya Cup na matatu ya Enterprise Cup kati ya 2000 na 2002. Anajivunia mataji mengi ya haiba kubwa kutokana na ufanisi wake binafsi na mafanikio ya Shujaa katika mapambano mbalimbali ya Raga ya Dunia.

Hadi kuteuliwa kwake katika wadhifa wa sasa katika Rugby League, Ayimba alikuwa kocha msaidizi kambini mwa Kenya Harlequins.

  • Tags

You can share this post!

Ighalo kuendelea kuwa ‘Shetani Mwekundu’ kwa...

Strathmore Leos kusajili wachezaji watano

adminleo