Bakken Bears anayopchezea Tylor Ongwae yanusia kuingia Klabu Bingwa ya mpira wa vikapu
NA GEOFFREY ANENE
NICOSIA, Cyprus:
BAKKEN Bears Aarhus, ambayo imeajiri Mkenya Tylor Okari Ongwae, imeanza kampeni ya kuingia Klabu Bingwa ya Mpira wa Vikapu barani Ulaya kwa kishindo baada ya kubwaga Hapoel Tel Aviv 91-71 mjini Nocosia nchini Cyprus hapo Septemba 23.
Bears ilidumisha kikosi Ongwae, Justin Dentmon, Darko Jukic, Ryan Evans na Michael Diouf kilichopigwa 96-91 katika mechi ya kujipima nguvu dhidhi ya mabingwa wa Ujerumani Alba Berlin mnamo Septemba 17.
Wafalme hao wa Denmark, ambao walikuwa wamelemea Rostock Seawolves kutoka Ujerumani 96-89 (Septemba 16) na London Lions kutoka Uingereza 105-88 (Septemba 6) katika mechi zingine za kirafiki, walianza vyema. Waliongoza robo ya kwanza kwa alama 6-0. Hata hivyo, waliachilia uongozi 13-16 kabla ya kujikakamua na kuenda mapumziko mafupi wakiwa juu pembemba 22-21.
Ilikuwa nipe-nikupe katika robo ya pili kabla ya Bears kufaulu kufungua mwanya wa alama tisa ikienda mapumziko marefu kifua mbele 45-36.
Bears ilirejea kipindi cha pili katili zaidi ikiongeza mwanya wa alama 16 na kuudumisha kabla ya Hapoel kuupunguza hadi alama 13 mwisho wa robo ya tatu ambayo ilishinda 73-56.
Zikisalia dakika sita na sekunde 30, Bears ilikuwa imefungua mwanya wa alama 17 ikiongoza 81-64 na haikukubali kukaribiwa tena na Hapoel.
Baada ya kulemea Hapoel katika nusu-fainali hiyo ya kwanza ya Kundi A, Bears itakutana na mshindi wa nusu-fainali ya pili kati ya Anwil Wloclawek (Poland) na Belfus Mons-Hainaut (Ubelgiji) katika fainali mnamo Septemba 25.
Bingwa wa kundi hili atatiwa katika Kundi A la Klabu Bingwa linalojumuisha Dinamo Sassari (Italia), Galatasaray Doga Sigorta (Uturuki), Iberostar Tenerife (Uhispania), Peristeri Winmasters (Ugiriki), Rytas (Lithuania), SIG Strasbourg (Ufaransa) na VEF Riga (Latvia).
Isiposhinda mechi za kuingia Klabu Bingwa, Bears itateremka katika ligi ya daraja ya pili (Europe Cup).