Michezo

Bandari ange kuzichapa na Cape Town City kirafiki

June 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Bandari FC imeratibiwa kucheza mechi ya kwanza ya kujipima nguvu dhidi ya timu ya Cape Town City nchini Afrika Kusini hii leo Jumatano.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Bandari FC Edward Oduor amesema anatarajia vijana hao wa kocha Benni McCarthy kuwapa mazoezi ya kutosha.

Cape Town City, ambayo iliwahi kuajiri mshambuliaji Mkenya Masoud Juma kati ya Januari mwaka 2018 na Agosti mwaka huo, ilikamilisha Ligi kuu ya Afrika Kusini iliyopita katika nafasi ya nne.

Bandari, ambao ni mabingwa wa Kenya wa Kombe la Ngao mwaka 2015 na 2019, waliondoka nchini Juni 22 kushiriki kambi ya mazoezi ya wiki moja nchini Afrika Kusini kujitayarisha kwa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Kagame Cup), Kombe la Mashirikisho la Afrika (CAF Confederation Cup) na Ligi Kuu.

Vijana wa kocha Bernard Mwalala pia wanatarajiwa kusakata mechi nyingine ya kirafiki nchini Afrika Kusini mnamo Alhamisi dhidi ya timu ambayo bado haijatambuliwa. “Kesho tunatarajia kujua timu ya pili tutakayocheza nayo,” alisema afisa huyo.

Ziara hiyo inadhaminiwa na Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) iliyoahidi itawazawidia wachezaji kwa kufanya ziara ya Afrika Kusini wakishinda taji la SportPesa Shield (Kombe la Ngao).

Katika mahojiano, Oduor aliambia Taifa Leo kuwa timu hiyo iliwasili Cape Town nchini Afrika Kusini siku ya Jumamosi usiku ikiwa na wachezaji wote isipokuwa sajili mpya Danson Chetambe kutoka Zoo FC, ambaye hati zake bado zinashughulikiwa.

Hata hivyo, orodha ya majina ya wachezaji na maafisa wa timu hiyo walioko Afrika Kusini bado haijatangazwa rasmi.

Naibu kocha Nassoro Mwakoba alifichua kuwa kikosi hakina majeraha isipokuwa mchezaji Bernard Odhiambo, ambaye anaendelea na matibabu.

Klabu ya Cape Town City inadhaminiwa na kampuni ya bahati nasibu ya SportPesa. Zilifanya mapatano ya miaka minne mwezi Agosti mwaka 2017.

Kampuni ya SportPesa inadhamini Ligi Kuu ya Kenya pamoja na klabu za Gor Mahia na AFC Leopards. Ilialika timu ya Bandari kushiriki makala ya tatu ya soka ya Afrika Mashariki ya SportPesa Cup nchini Tanzania.

Bandari ilifika fainali, lakini ikapoteza dhidi ya Kariobangi Sharks mapema mwaka 2019.

Kuikabili Everton

Mshindi wa soka hiyo inayokutanisha klabu za Kenya na Tanzania hupata fursa ya kukabiliana na timu ya Everton kutoka Ligi Kuu ya Uingereza.

Gor ilishinda makala mawili ya kwanza na kukutana na Everton mwaka 2017 jijini Dar es Salaam na mwaka 2018 mjini Liverpool. Ilipoteza 2-1 na 4-0 mtawalia.

Sharks itakaribisha Everton katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani mnamo Julai 7. Bandari inarejea katika mashindano ya Afrika baada ya kukosa makala matatu mfululizo. Ilibanduliwa kutoka Kombe la Mashirikisho la Afrika katika awamu ya kuingia raundi ya kwanza mwaka 2015.