• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Bandari FC yatoka sare 2-2 dhidi ya wenyeji wao Cape Town City

Bandari FC yatoka sare 2-2 dhidi ya wenyeji wao Cape Town City

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kombe la Ngao (SportPesa Shield) mwaka 2015 na 2019 Bandari FC wametoka 2-2 dhidi ya wenyeji wao Cape Town City katika mechi yao ya kwanza ya kirafiki nchini Afrika Kusini, Jumatano.

Vijana wa kocha Bernard Mwalala, ambao wako nchini Afrika Kusini kwa matayarisho ya msimu 2019-2020, walipata mabao kupitia kwa Mganda William Wadri na Benjamin Mosha.

Cape Town City, ambayo inanolewa na shujaa wa zamani wa Afrika Kusini Benni McCarthy, ilitikisa nyavu za Bandari kupitia kwa wachezaji Chris David na Siphelele Mthembu.

Bandari, ambayo inatarajiwa kusakata mechi yake ya pili na mwisho ya kirafiki hapo Juni 27 kabla ya kurejea nyumbani, inajiandaa kukutana na Azam (Tanzania), Mukura (Rwanda) na KCCA (Uganda) katika mechi za Kundi B za soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Kagame Cup) mwezi Julai nchini Rwanda.

Timu zingine zitakazoshiriki Kagame Cup ni Rayon Sports (Rwanda), TP Mazembe (DR Congo), KMC (Tanzania) na Atlabara (Sudan Kusini) katika Kundi A, APR (Rwanda), Green Buffaloes (Zambia), Proline (Uganda) na Heegan (Somalia) ziko katika Kundi C nazo Gor Mahia (Kenya), DC Motema Pembe (DR Congo), KMKM (Zanzibar) na AS Ports (Djibouti) zinaunda Kundi D.

Gor ilishinda Kagame Cup mwaka 1976, 1977, 1980, 1981 na 1985, APR mwaka 2004, 2007 na 2010, KCCA mwaka 1978, Azam (2015 na 2018) nayo Rayon (1998).

Bandari, ambayo itakuwa ikitafuta taji lake la kwanza kabisa la Cecafa, pia inajiandaa kurejea katika Kombe la Mashirikisho la Afrika (Confederation Cup) tangu mwaka 2015 baada ya kufuzu kushiriki msimu 2019-2020 kwa kuchapa Kariobangi Sharks katika SportPesa Shield mnamo Juni 1.

Vijana wa Mwalala, ambao pia walimaliza Ligi Kuu msimu 2018-2019 katika nafasi ya pili nyuma ya Gor, wanajipiga msasa wakitumai kufukuzia taji lao la kwanza kabisa ligini.

Bandari FC dhidi ya Cape Town City. Picha/ Hisani
  • Tags

You can share this post!

AFCON 2019: Kenya si kali kuliko Tanzania – Amunike

Fataki kulipuka Senegal na Algeria wakipapurana

adminleo