• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Bandari tayari kuinyamazisha Chemelil Sugar

Bandari tayari kuinyamazisha Chemelil Sugar

Na ABDULRAHMAN SHERIFF na JOHN ASHIHUNDU

NAIBU Kocha wa Bandari FC, Ibrahim Shikanda amesema jana Ijumaa kuwa ni lazima wapate ushindi dhidi ya Chemelil Sugar timu hizo zitakapokutana kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) itakayochezwa uwanjani wa Mbaraki Sports Club hivi leo Jumamosi.

Shikanda alitamba kuwa wana uhakika watashinda mechi hiyo hasa kwa kuwa watakuwa nyumbani. “Sioni sababu ya kutoshinda tukiwa nyumbani. Tunataka tumalize mechi tukiwa na alama zote tatu,” akasema.

Alisema tamaa yake kubwa ni kuwa wachezaji wao wameshiba kwa mazoezi na wamepata uzoefu zaidi kutokana na ziara yao ya mechi mbili Tanzania ambapo walifungwa 1-0 na Simba jijini Dar es Salaam na kulipa kisasi kwa kuishinda Coastal Union 1-0 mjini Tanga.

Shikanda aliwapongeza mashabiki wao na kuwashangilia kila wanapocheza mechi zao za ligi, mashindano na kirafiki na akawaomba wazidi kufurika uwanjani hivi leo kuwapa motisha wachezaji.

Mkufunzi huyo alisema kambi ya mazoezi ya kujiandaa kwa mechi yao ya Caf Confederation Cup dhidi ya Horoya AC ya Equatorial Guinea hapo Jumapili wiki ijayo ya Oktoba 27, imekuwa nzuri.

Timu ya Bandari inatarajia kuondoka nchini Jumatano ya wiki ijayo kuelekea Equatorial Guinea kupambana na Horoya AC, amesema Afisa Mkuu wa Bandari FC, Edward Oduor.

Alisema wanatarajia kuondoka kuelekea huko Guinea Jumatano baada ya kucheza mechi yao ya mwisho ya kujipima nguvu siku ya Jumapili dhidi ya timu ya Ligi ya Taifa Daraja la Pili, Sparki Youth FC.

Mechi yao hiyo na Sparki Youth itakuwa ni ya kugombea Kombe la Mashujaa na itachezwa uwanja wao wa Mbaraki Sports Club. “Tunatarajia mashabiki wengi watajitokeza kuishuhudia timu yao ikikamilisha mechi za maandalizi,” akasema.

Baraza la Kusimamia Ligi Kuu (KPL) limeamua kwamba mechi zote tisa za wikendi hii zitaendelea kama ilivyopangwa, licha ya vilio vya uhaba wa pesa kwa timu husika.

  • Tags

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Ninashuku anamgawia mpenziwe wa zamani

Ghasia zapangua gozi la El Clásico

adminleo