Bandari yatoka nyuma kuilima Tusker
Na GEOFFREY ANENE
BANDARI FC ilitoka nyuma bao moja na kuzima wageni wake wa Tusker FC katika mechi ya kusisimua ya Ligi Kuu uwanjani Mbaraki mjini Mombasa, Alhamisi.
Ushindi huu uliopatikana kupitia mabao ya Yema Mwana na Shaban Kenga unafanya Bandari kuruka mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka na kuziba mwanya kati yake na viongozi Gor Mahia hadi nane.
Mwana aliweka Bandari mabao 2-1 juu mapema katika kipindi cha pili baada ya kunufaika na mawasiliano mabaya upande wa Tusker kati ya beki na kipa aliyepigiwa pasi ya nyuma. Raia huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliiba pasi hiyo na kufunga.
Tusker ndiyo ilitangulia kuona lango. Eugine Asike alipata mpira uliotemwa na kipa Farouk Shikalo baada ya David Naftali kupiga kichwa na kuufunga dakika ya 22.
Hata hivyo, bao hili liliamsha wenyeji Bandari ambao walishambulia ngome ya Tusker vilivyo na kusawazisha 1-1 kabla ya mapumziko kupitia kwa Shaban Kenga dakika ya 33.
Kenga alipokea krosi kutoka kwa Mganda William Wadri baada ya shuti la kutoka mbali la Abdallah Hassan kuzuiwa.
Wadri alipumzishwa dakika ya 76 na kocha Bernard Mwalala akajaza nafasi yake na mchezaji Benjamin Mosha. Badiliko hili liliishia kuwa la busara kwani Mosha alizamisha kabisa chombo cha Tusker pale alipotikisa nyavu dakika ya 90 baada ya frikiki ya Hassan kutemwa na kipa.
Mabingwa watetezi Gor wanaongoza ligi hii ya klabu 18 kwa alama 66. Walipoteza nafasi ya kukaribia taji pale walipokung’utwa na Nzoia Sugar 1-0 mjini Mumias mnamo Jumatano. Baada ya kunyima Tusker ushindi msimu huu, Bandari imevuna alama 58.
Sofapaka inafuatia katika nafasi ya tatu kwa alama 56, huku Kakamega Homeboyz na washindi wa mwaka 2008 Mathare United wakifunga mduata wa tano-bora kwa alama 51 na 49, mtawalia.