Michezo

Barcelona yalia na kusaga meno huku Dortmund wakipepea Uefa

April 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BARCELONA, Uhispania

KOCHA Xavi Hernandez wa Barcelona amesema maamuzi mabaya ya refarii yalisababisha timu yake kubanduliwa na Paris Saints-Germain (PSG) katika robo-fainali ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA).

Kwenye mechi hiyo iliyochezewa Olympic Stadium Lluis, Jumanne usiku, Barcelona walifunga mapema na kuongoza kabla ya PSG kutoka nyuma na kuibuka na ushindi wa jumla wa 6-4 kutokana na mabao ya haraka kupitia kwa Kylian Mbappe (2) na Ousmane Dembele.

Katika robo-fainali nyingine iliyochezwa Jumanne, wenyeji Borussia Dortmund walitandika Atletico Madrid ya Uhispania 4-2 na kufuzu kwa nusu-fainali kwa jumla ya mabao 5-4.

Dortmund walipata mabao yao kupitia kwa Julian Brandt dakika ya 34, Ian Maatsen 39′, Fullkrug 71′ na Sabitzer 74′.

Mats Hummels wa Dortmund alifungia Madrid bao la kwanza dakika ya 49 katika juhudi za kujaribu kuokoa hatari langoni, kabla ya Angel Correa kuongeza la pili dakika ya 64.

Ugani Olympic Stadium Lluis, PSG waliokuwa chini kwa 3-2 katika kipindi cha kwanza, walirejea kwa kishindo na kutinga nusu-fainali baada ya Barcelona kuchanganyikiwa mechi iliposhika kasi.

Xavi aliyelishwa kadi nyekundu kwa kumfokea mwamuzi anadai refa, Istavan Kovacs kutoka Romania alifanya makosa kwa kumtoa Ronald Aruajo kwa kadi nyekundu pamoja na kuwapa PSG penalti, mbali na kupiga kadi za manjano wachezaji wake kadhaa adhabu ambazo anaamini zilienda kinyume na sheria za soka.

“Mwamuzi alituonea hadharani. Nilimwambia utendaji kazi wake ulikuwa duni,” Xavi alisema kupitia Movistar Plus.

“Tumekerwa sana kwa sababu morali yetu ilishuka mara tu alipotoa kadi nyekundu. Tulipokuwa 11 kwa 11, tulikuwa tukicheza vizuri kuliko wapinzani wetu. Refarii alitoa kadi kiholela. Alitoa kadi kiholela na kutuharibia mchezo. Mechi kama hii haistahili mwamuzi wa aina hiyo.”

Barcelona walilemewa baada ya Aruajo kutolewa mapema kwa kadi nyekundu. Makosa mengi yalianza kutokea kwenye eneo la hatari la Barcelona, likiwemo la Joao Cancelo kumuangusha Dembele katika eneo la hatari na kuchangia penalti iliyofungwa na Mbappe.

Chukizo

“Ni jambo la kuchukiza kwamba baada ya maandalizi ya msimu mzima, juhudi zetu zinaangamizwa na uamuzi mbaya,” Xavi alisema kupitia kwa CBS.

Lakini akizungmzia kuhusu mchezo huo, mshambuliaji wa zamani, Thierry Henry aliyewahi kuchezea Barcelona na Arsenal miongoni mwa timu nyingine, alisema wachezaji wanapaswa kujihadhari kufanya makossa katika mechi kubwa kama hiyo.

“Unapofanya makosa holela katika mechi ya kiwango hiki, unaadhibiwa papo hapo. Hiyo ilikuwa penalti ya wazi,” aliongeza Mfaransa huyo.

Barcelona walitarajiwa kuwa na kazi rahisi kwenye mechi hiyo ya marudiano baada ya kuondoka Paris na ushindi wa 3-2, na walikuwa na mwanzo mzuri baada ya Rafhinha kufunga bao la kwanza.

“Mambo yangekuwa sawa iwapo tungecheza wachezaji 11 dhidi ya 11. Mchezaji anaweza kuonyeshwa kadi nyekundu akifanya makossa, lakini hii aliyopewa Aruajo haikustahili.”

Ilikuwa mechi ambayo mwamuzi huyo alitoa jumla ya kadi 12, mbali na mabao matano yaliyofungwa usiku huo, pamoja na penalti.