Michezo

Barua ya Samuel Eto’o kujiuzulu yakataliwa

February 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2


JOHN ASHIHUNDU NA MASHIRIKA

KAMATI Kuu ya Shirikisho la Soka nchini Cameroon (FECAFOOT) imekataa kuidhinisha barua ya kujiuzulu kwa rais wa shirikisho hilo, Samuel Eto’o.

Eto’o aliwasilisha barua ya kujiuzulu siku chache tu baada ya timu ya taifa hilo maarufu kama Indomitable Lions kuondolewa mapema katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazoendelea nchini Ivory Coast.

Cameroon ambayo ilifuzu kimungumungu kwa raundi ya 16–bora, iling’olewa na Nigeria kwa kichapo cha mabao 2-0 katika hatua hiyo. Eto’o aliyechaguliwa rais mnamo Desemba 2021 alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri walioenda Ivory Coast kushangilia Indomidale Lions.

Alionekana pichani akifurahia timu hiyo ilipotinga hatua hiyo ya 16-bora, lakini CAF imesema inamchunguza kwa madai ya kuhusika katika upangaji wa matokeo ya mechi, vitisho kwa wachezaji, matusi na kuchochea fujo, madai ambayo mawakili wake wamekanusha.

Mshambuliaji huyo aliyefungia Cameroon mabao 56 katika mechi 118 za kimataifa akiwa mchezaji, ana sifa sufufu duniani kutokana na umaarufu wake alipochezea klabu za Barcelona, Inter Milan na Chelsea.

Umaarufu wake mwingine ni pamoja na ushindi wake Kombe la Mabingwa barani Ulaya mara tatu na kombe la Afcon mara mbili.

Imeripotiwa kwamba Eto’o anavurugana mara kwa mara na kipa chaguo la kwanza Andre Onana wa Manchester United ambaye hapo awali aliondolewa kikosini wakati wa Kombe la Dunia nchini Qatar, kabla ya kustaafua, na baadaye kubadilisha msimamo huo.

Eto’o vile vile alidaiwa kufokeana na shabiki nchini Qatar wakati wa fainali za Kombe la Dunia na kutishia baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho.

Lakini baada ya kuongoza kikao cha Fecafoot kilichofanyika jijini Younde, Jumatatu kujadili matokeo duni ya Indomitable Lions, Eto’o aliwasilisha barua ya kujiuzulu, lakini kikao hicho kwa pamoja kilikataa kuidhinisha barua hiyo.

“Sote tuna imani kwake, na tunataka aendelee na mipango yake ya kuimarisha soka nchini kama alivyoahidi baada ya kuchaguliwa.”

Cameroon inashikilia nafasi ya 46 katika viwango vya Fifa, huku ikiwa katika nafasi ya saba barani Afrika. Timu hiyo ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye fainali za Afcon 2021, kabla ya baadaye kubanduliwa katika hatua ya makundi wakati wa Kombe la Dunia la 2022 nchini Qatar.