Michezo

Basi la Benfica lavamiwa, wachezaji wajeruhiwa

June 7th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

WACHEZAJI wawili wa Benfica wamepelekwa walijeruhiwa na kupelekewa hospitalini kufuatia tukio la basi lao kuvamiwa mwishoni mwa mechi yao ya kwanza tangu kurejelewa kwa Ligi Kuu ya Ureno.

Wawili hao ni Julian Weigl wa Ujerumani na Andrija Zivkovic wa Serbia ambao waliumizwa kwa mawe na vifaa butu walivyorushiwa wakiwa ndani ya basi la timu.

Benfica ambao ni mabingwa wa soka ya Ureno walipoteza fursa ya kuwapiku FC Porto kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu baada ya kulazimishiwa sare tasa na Tondela.

Idadi kubwa ya mashabiki walikuwa wamekongamana nje ya uwanja wa Estadio da Luz kuwatilia shime wanasoka wa vikosi vyao.

Basi la Benfica lilishambuliwa kwenye barabara inayounganisha uwanja wa Estadio da Luz na eneo la wanasoka kufanyia mazoezi.

“Benfica wanakemea tukio hili la wahalaifu kuvamia basi, kulipiga kwa mawe na kuwajeruhi wachezaji. Tumeanzisha mchakato wa kuwasaka wahalifu hao na kuwachukulia hatua kali za kisheria,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Benfica.

Zikisalia mechi tisa zaidi kwa kampeni za Ligi Kuu ya Ureno kukamilika rasmi msimu huu, Porto na Benfica wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 60 kila mmoja. Braga wanashikilia nafasi ya tatu kwa pointi 46, tatu zaidi kuliko Sporting Lisbon wanaofunga mduara wa nne-bora baada ya kila kikosi kusakata jumla ya mechi 25.