Bayern yasajili Choupo-Moting na Douglas Costa
Na CHRIS ADUNGO
BAYERN Munich wamejinasia huduma za fowadi raia wa Cameroon, Eric Maxim Choupo-Moting, 31, kwa mkataba wa mwaka mmoja.
Nyota huyo mzawa wa Hamburg, Ujerumani hakuwa na klabu baada ya mkataba wake na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kutamatika rasmi mwishoni mwa Septemba 2020.
Mbali na Choupo-Moting, mwanasoka mwingine ambaye amesajiliwa na Bayern ni mfumaji matata raia wa Brazil, Douglas Costa ambaye ameagana na Juventus kwa mkopo.
“Nani asingependa kuchezea Bayern? Kuingia katika sajili rasmi ya kikosi hicho ni fahari na tija kubwa. Hiki ni kikosi kinachojivunia historia ndefu ya mafanikio katika soka ya Ujerumani na bara Ulaya,” akasema Choupo-Moting.
Hadi alipojiunga na PSG bila ada yoyote mnamo 2017-18, Choupo-Moting aliwahi pia kuchezea Hamburg, Mainz na Schalke nchini Ujerumani, kisha akafungia Stoke City mabao matano kabla ya kikosi hicho kushushwa ngazi katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2018.
Japo hakuwa na uhakika wa kuwajibishwa katika kikosi cha kwanza cha PSG mara kwa mara, Choupo-Moting alifunga bao muhimu lililowawezesha PSG kutoka nyuma na kubandua Atalanta ya Italia kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2019-20.
Alikuwa pia sehemu ya kikosi cha PSG kilichopepetwa na Bayern 1-0 kwenye fainali ya UEFA msimu uliopita wa 2019-20 jijini Lisbon, Ureno.
“Ni mwanasoka anayejivunia tajriba pevu katika soka ya bara Ulaya. Pia ana uzoefu mkubwa katika soka ya Ujerumani. Isitoshe, ametua ugani Allianz Arena bila ada yoyote,” akasema mkurugenzi wa spoti kambini mwa Bayern, Hasan Salihamidzic.
Costa aliwahi kuchezea Bayern kati ya 2015 na 2017 ambapo aliwafungia mabao 14 kutokana na mechi 77 na kuwasaidia kutia kapuni mataji matatu ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).
“Niliwahi kujivunia misimu ya kuridhisha kambini mwa Bayern na nina hakika nitaendelea kutwaa mataji zaidi nikivalia jezi zao,” akasema Costa.