• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Beki Joseph ‘Crouch’ Okumu asema Simba SC hawawezi kumng’oa Uswidi

Beki Joseph ‘Crouch’ Okumu asema Simba SC hawawezi kumng’oa Uswidi

Na CHRIS ADUNGO

BEKI matata wa Harambee Stars, Joseph ‘Crouch’ Okumu, 23, amefutilia mbali tetesi zinazomhusisha na uwezekano wa kuyoyomea nchini Tanzania kuvalia jezi za Simba SC msimu huu wa 2020-21.

Kwa mujibu wa difenda huyo wa IF Elfsborg nchini Uswidi, Simba ambao walitia kapuni jumla ya mataji matatu msimu uliopita, hawajawasilisha ofa yoyote kwa waajiri wake wala wakala wake licha ya miamba hao wa soka ya Tanzania kusisitiza kwamba “mazungumzo kati yao na Okumu yako katika hatua za mwisho mwisho”.

Katika taarifa yao, Simba ambao pia wanampa hifadhi kiungo Francis Kahata wa Harambee Stars, walikiri kuwa wanazihemea huduma za Okumu kadri wanavyolenga kutia fora zaidi katika kampeni za Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) msimu ujao.

Simba waliobanduliwa mapema kwenye kipute hicho katika msimu wa 2019-20, walianza mchakato wa kujisuka upya wikendi iliyopita kwa kujinasia maarifa ya kiungo matata mzawa wa Ghana, Bernard Morrison aliyekatiza uhusiano wake na Yanga SC ambao ni watani wa tangu jadi wa Simba katika soka ya Tanzania.

Simba pia wako pua na mdomo kumsajili beki matata wa timu ya taifa ya Harambee Stars, Joash Onyango ambaye kwa kutua Simba, ataungana na waliokuwa wachezaji wenzake kambini mwa Gor Mahia, Kahata na Meddie Kagere. Ingawa walikuwa wakimnyemelea pia kiungo na nahodha wa Gor Mahia, Kenneth Muguna, huenda ujio wa Morrison ukasitisha mpango huo.

Muguna ambaye pia amewahi kuchezea Western Stima na FK Tirana ya Albania, anahusishwa sasa na uwezekano mkubwa wa kuingia katika sajili rasmi ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ay Petro Atletico ya Angola ambao pia waliwahi kumsajili fowadi Jacques Tuyisenge kutoka Gor Mahia.

Okumu pia ametilia shaka uwezo wa Simba kushawishi Elfsborg kumwachilia au hata kulipia mkataba wa miaka miwili alionao na miamba hao wa Uswidi.

Beki huyo wa zamani wa Free State Stars ya Afrika Kusini, amekuwa tegemeo kubwa kambini mwa Elfsborg tangu akatize uhusiano na Real Monarchs ya Amerika mwaka 2019.

Licha ya umri wake mdogo, Okumu aliridhisha sana ndani ya jezi za Harambee Stars kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri. Alitegemewa sana na kocha Sebastien Migne katika mechi za makundi dhidi ya Algeria, Tanzania na Senegal.

You can share this post!

Wawili wajeruhiwa baada ya V8 kugonga nguzo za barabarani

Balala ahakikishia wawekezaji sekta ya utalii wizara...

adminleo