Beki Samuel Umtiti augua Covid-19
Na CHRIS ADUNGO
BEKI Samuel Umtiti wa Barcelona, 26, ameugua ugonjwa wa Covid-19.
Nyota huyo mzawa wa Ufaransa hajawahi kuwajibishwa katika mchuano wowote tanngu Julai 2020 baada ya kupata jeraha la goti.
Kwa mujibu wa Barcelona, Umtiti ambaye anahusishwa pakubwa na uwezekano wa kutua Arsenal muhula huu, hakuonyesha dalili zozote za kuwa na virusi vya corona alipofanyiwa vipimo vya afya.
“Klabu imewataarifu maafisa wa afya na vinara husika kambini mwa Barcelona kuhusiana na tukio hilo na kwa sasa watu wote waliotangamana na Umtiti wanatafutwa ili kudhibiti msambao zaidi wa virusi hivyo,” ikasema sehemu ya taarifa ya miamba hao wa soka ya Uhispania.
Kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Bayern Munich kwenye robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 14, 2020, Barcelona walikuwa wameripoti kwamba mwanasoka mmoja kambini mwao alikuwa na vieusi vya corona.
Ingawa jina la mchezaji huyo lilibanwa wakati huo, sasa Barcelona wamefichua kwamba sogora huyo ni beki Jean-Clair Todibo, 20.
Chipukizi huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji tisa wa Barcelona waliokuwa wakirejea kambini kujiandaa kwa mapambano ya msimu ujao wa 2020-21.